WADAU WAITAKA TAMISEMI KUWAWEZESHA MAAFISA UTAMADUNI




Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) Ghonche Materego akitoa ufafanuzi wa masuala mbalimbali kwenye Jukwaa la Sanaa wiki hii.Katikati ni Ofisa Utamaduni Wilaya ya Ilala, Kitogo , Kulia ni Mwalimu Rashid Masimbi ambaye pia ni Mkurugenzi wa Kituo cha Sanaa za Maonyesho Tanzania akichangia mada kwenye Jukwaa la Sanaa. Wakongwe wakichangia mada kwa nguvu zote kwenye Jukwaa la Sanaa -Waziri Ally kutoka bendi ya Muziki Kilimanjaro ‘Njenje’ na anayeonekana katika picha chini kushoto ni Hamza Kalala ‘ Mzee wa Madongo’ kutoka bendi ya Bantu Group.

Na Aristide Kwizera


Wadau wa Sanaa wameiomba Wizara ya Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kuwawezesha maafisa utamaduni ili kusukuma shughuli za sanaa na utamaduni katika ngazi za wilaya na mikoa. Wakizungumza kwenye Jukwaa la Sanaa linalofanyika kila Jumatatu kwenye Ukumbi wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), wadau hao walisema kwamba,maafisa utamaduni wamekuwa wakipewa bajeti ndogo kiasi cha kufanya shughuli za sanaa na utamaduni kushindwa kuendelea na kukwama kabisa. Aidha, walilalamikia hali ya Maafisa Utamaduni kuwa chini ya Idara ya Elimu na Mafunzo iliyo chini ya Afisa Elimu wa wilaya hali ambayo imewafanya wakose gawio la kutosha la bajeti kwa ajili ya maendeleo ya sekta ya utamaduni badala ya wao kuwa na bajeti maalum kwa ajili ya kushughulikia sekta hiyo muhimu.


“Maafisa Utamaduni wamekuwa wakipewa fedha kidogo sana,hata ofisi zao hazieleweki kwani zimefichwa ndani ya idara ya elimu na mafunzo ya wilaya.

wakikumbukwa nyakati za Mwenge tu kwa kupewa fedha za kukamilisha shughuli hiyo.Kwa hali hii sekta ya utamaduni itapiga hatua kweli?” alihoji Nkwama Bhallanga ambaye ni Mjumbe wa Shirikisho la Sanaa za Maonyesho nchini.

Alizidi kueleza kwamba,sekta ya sanaa imekuwa ikishughulikiwa na wizara tatu tofauti akimaanisha ya Viwanda na Masoko,TAMISEMI na ile ya Habari,Vijana,Utamaduni na Michezo hali ambayo imekuwa ikisababisha migongano ya kiutendaji na ukosefu wa usimamizi wa moja kwa moja wa sekta hii katika wizara moja.

Awali Katibu Mtendaji wa BASATA,Ghonche Materego alisema kwamba,kumekuwa na changamoto nyingi katika kuwafikia wasanii walioko wilayani na hata kusukuma maendeleo ya sekta ya utamaduni kwani maafisa utamaduni wamekuwa chini ya idara elimu na mafunzo ambapo wamekuwa wakipata fedha ndogo sana kwa ajili ya shughuli zao.

“Fedha za usajili wa wasanii mathalan, inabidi zirudi kwa wasanii walioko wilayani lakini inakuwa ngumu kwa sababu maafisa utamaduni wako chini ya Afisa Elimu hivyo fedha hazitaweza kugharamikia sanaa bali shughuli zingine tofauti.

Hii ndiyo changamoto iliyopo na inapaswa kutatuliwa.

Aliongeza kwamba,BASATA limeshatuma waraka maalum kwa wakurugenzi wa wilaya kuomba kuwe na akaunti maalum ya sanaa ili fedha zitakazotumwa ziwe zinatumika kwa wasanii na sekta ya sanaa pekee lakini hadi sasa hilo halijafanyika. Katika Jukwaa hilo la sanaa,Afisa Utamaduni wa Wilaya ya Ilala Shani Kitogo aliwasilisha mada juu ya Ugharamiaji na uendeshaji wa shughuli za sanaa na Utamaduni katika ngazi ya Wilaya ambapo aliibua changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na hiyo ya maafisa utamaduni kutokuwezeshwa.

Post a Comment

0 Comments