TIKETI ZA MECHI YA TAIFA STARS Vs AFRIKA KATI KUANZA KUUZWA MACHI 24


Mechi ya mchujo ya Kombe la Mataifa ya Afrika (CAN) kati ya Taifa Stars na Jamhuri ya Afrika ya Kati itachezwa Machi 26 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ambapo viingilio ni kama ifuatavyo; Viti vya Kijani na Bluu sh. 3,000, Viti vya Rangi ya Chungwa (Orange straight and curve) sh. 5,000, VIP C sh. 10,000, VIP B sh. 20,000 na VIP A sh. 40,000.
Tiketi zitaanza kuuzwa Machi 24 mwaka huu saa 2 asubuhi katika vituo vifuatavyo; Shule ya Sekondari Benjamin Mkapa, Big Bon Msimbazi (Kariakoo), Mgahawa wa Steers (Mtaa wa Samora/Ohio), Kituo cha Mafuta OilCom (Ubungo), Uwanja wa Uhuru, Kituo cha Mafuta Kobil (Buguruni) na Kituo Kidogo cha Polisi Tandika Mwisho.

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) litatoa asilimia moja ya mapato yatakayopatikana katika mechi hiyo kusaidia waathirika wa maafa ya mabomu ya Gongo la Mboto.

NAULI LIGI KUU YA VODACOM
Klabu zote 12 ambazo timu zao zinashiriki katika Ligi Kuu ya Vodacom zimelipwa mgawo wa mwisho wa nauli kwa msimu huu wa 2010/2011. Kila klabu imepokea hundi ya sh. milioni 5.2. Kwa msimu mzima kila klabu imepata jumla ya sh. milioni 24.5 kwa ajili ya nauli. Fedha hizo ni sehemu ya udhamini wa Kampuni ya Vodacom kwenye Ligi Kuu.

MIGOGORO KWA WANACHAMA
TFF inawakumbusha wanachama wake (vyama vya mpira wa miguu vya mikoa, vyama shiriki na klabu za Ligi Kuu) kuwa haitambui mapinduzi ya uongozi kwani ni kinyume cha katiba zao. Kwa wanachama ambao kuna nafasi zilizo wazi baada ya viongozi kujiuzulu wanatakiwa kuzijaza kwa kufanya uchaguzi.

Boniface Wambura
Ofisa Habari

Post a Comment

0 Comments