Mwanamuziki kijana na mahiri kutoka Tanzania, Diamond, leo ametangazwa kuwania tunzo maarufu ya muziki barani Afrika ya MTV Africa Music Awards (MAMA 2010) na hivyo kuwa mwanamuziki pekee kwa mwaka huu kuwania tuzo hizo kutoka hapa nchini, tuzo ambazo zinatolewa na MTV na kudhaminiwa na Zain.
Wanamuziki mbalimbali wanaowania tuzo za MAMA 2010 barani Afrika, ambao wengi wao ni wanamuziki vijana wenye vipaji vya hali ya juu, wamatangazwa usiku wa kuamkia leo katika hafla maalum iliyofanyika jijini Lagos, Nigeria na kuhudhuriwa na wanamuziki, wasanii mbalimbali pamoja na watu maarufu na mashuhuri wakiwemo 2Face, Sasha na Mo Cheddah. Majina ya wanaowania tuzo mwaka huu yaliwekwa bayana na Alex Okosi - Makamu wa Rais Mwandamizi wa MTV Africa, Adre Bayers – Afisa Masoko Mkuu wa Airtel Afrika na Rajan Swaroop – Afisa Mtendaji Mkuu wa Zain Nigeria.
Kwa upande wa wasanii kutoka Afrika ya Mashariki, kuna jumla ya wasanii watano watakaowania tuzo hii ya MAMA 2010 ambao wanatoka Tanzania, Kenya na Uganda. Muimbaji wa miziki ya Injili kutoka Kenya, Daddy Owen, kwa mara ya kwanza ameingia katika kinyang’anyiro cha tuzo hizi katika kundi la ‘Best Anglophone’ wakati msanii wa Hip Hop kutoka nchini humo, P-Unit akichuana katika kundi la ‘Best Group’ na Muthoni katika kundi la ‘Brand:New’.
Kutoka nchini Uganda, kikundi cha Radio and Whisle kwa mara ya kwanza kinaingia katika kuwania tuzo hizi katika kundi la ‘Best Group’ na mtanzania pekee katika kuwania tuzo hizi, Diamond, akichuana katika kundi la ‘Brand:New’.
Nigeria ndio nchi pekee ambayo imeingiza wasanii wake kuwania tuzo nyingi zaidi mwaka huu. Jumla ya tuzo 13 zinawaniwa na wasanii kutoka nchini humo ikiwa ni pamoja na P-Square (Msanii Bora wa Mwaka, Kundi Bora la Mwaka na Video Bora ya Mwaka) na 2Face (Mwanamuziki Bora wa Kiume na Mwanamuziki Bora wa Mwaka). Pia yumo mwanamuziki Wande Coal ambaye atachuana kuwania tuzo ya Mwanamuziki Bora kutoka nchi Zinazozungumza Kiingereza – Anglophone namoja na ile ya Mwanamuziki Bora wa Kiume.
Banky W, pia kutoka Nigeria atawania tuzo mbili tofauti mwaka huu, ikiwemo ya Wimbio Bora wa Mwaka pamoja na Video Bora ya Mwaka. Wanamuziki wa kike kutoka nchini humo, Nneka na Sasha watakuwa wakiwania tuzo ya Mwanamuziki Bora wa Kike wa kati Mo Cheddah akiwanua katika kundi la ‘Brand:New’.
D’Banj, ambaye kwa mara nne tofauti ameshinda tuzo za MAMA hapo awali, mwaka huu anaingia tena katika kinyang’anyiro hiki kwa kuwania tuzi ya Wimbo Bora wa Mwaka kupitia kibao chake cha ‘Fall in Love’.
Kundi la wasanii la JOZI kutoka Afrika Kusini, ambao mwaka 2008 waliibuka kuwa Watumbuizaji Bora wa ‘Live’, mwaka huu wanaingia tena ili kushindania tuzo ya Msanii Bora wa Mwaka. Wasanii wengine 6 kutoka Afrika Kusini pia watawania tuzo katika makundi mbalimbali, wakiwemo Teargas (Kundi Bora), JR (Wimbo Bora wa Mwaka), Black Coffee (Mwanamuziki Bora wa Kiume), Big Nuz (Muziki Bora – Anglophone), Liquideep (Wimbo Bora wa Mwaka) na Parlotones (Video Bora ya Mwaka).
Naye Faly Ipupa, ambaye pia atakuwa akitumbuiza katika onyesho la MAMA 2010, pia amependekezwa kuwania tuzo nne tofauti mwaka huu. Mwanamuziki huyu mahiri kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) atawania tuzo za Mwanamuziki Bora wa Mwaka, Mwanamuziki Bora wa Kiume, Video Bora pamoja na Muziki Bora – Francophone. Vile vile kutoka nchini humo, yumo mwanamuziki Barbara Kanam anayewania tuzo ya Mwanamuziki Bora wa Kike.
Baada ya Samini kuiwakilisha vema Ghana mwaka jana, mwaka huu msanii Sarkodie, kwa mara ya kwanza anaingia katika tuzo za MAMA kuwania katika kundi la Mwanamuziki Bora – Anglophone.
Kwa upande wa wanamuziki wa kimataifa, wasanii mahiri kutoka Marekani, Rihanna, Eminem, Drake pamoja na Rick Ross watachuana vikali katika kuwania tuzo ya kundi la Mwanamuziki Bora wa Kimataifa katika muziki wa Kisasa.
Kwa mwaka huu, kuna tuzo mbili zaidi katika MAMA, na hivyo kupanua wigo na maeneo zaidi ya ushindani kwa wanamuziki. Tuzo kwa Muziki Bora – Francophone kumeziwezesha cnhi kama Gabon kuingia katika tuzo hizi kwa mara kwanza kwa kuwakilishwa na Ba Ponga huku mwanamuziki anayewika kwa sasa kutoka nchini Senegal – Awadi pamoja na DJ Araft kutoka Ivory Coast wakiingia kwa mara ya kwanza kuwania tuzo hizi.
Tuzo nyingine iliyoongezeka na kuongeza hamasa katika MAMA 2010 ni ‘Best Lusophone’ na kuziwezesha nchi za Angola na Msumbiji kushiriki kwa mara ya Kwanza. Wanamuziki Capo Snoop na Paul G kutoka Angola pamoja na waimbaji Hip Hop kutoka Msumbiji – Lizha James na Dama do Bling watachuana kuwania tuzo katika kundi la ‘Best Lusophone’.
Akizungumza wakati wa kutaja wanamuziki watakaowania tuzo za MAMA 2010, Alex Okosi, Makamu wa Rais Mwandamizi wa MTV Africa amesema “Tuzo za MAMA mwaka huu zinahusisha wanamuziki kutoka nchi nyingi zaidi, ukilinganisha na miaka ya nyuma na hivyo kudhihirisha wazi kukua zaidi kwa muziki wa Afrika. Kuwepo kwa wanamuziki wanaotoka nchi zinazozungumza Kireno na Kifaransa kunazidi kuongeza chachu ya ushindani wa tuzo hizi kwa wanamuziki. TUnawapongeza wanamuziki wote waliochaguliwa kushindania tuzo hizi na tunawatakia mafanuikio mema hapo Disemba 11 jijini Lagos”.
Naye Adre Bayers, ambaye ni Afisa Masoko Mkuu wa Airtel barani Afrika, ameongeza kuwa “kutangazwa kwa wanamuziki hawa leo hii, ambao watachuana kuwania tuzo za MAMA 2010 kunaonyesha bayana ni kwa kiasi gani muziki una nguvu na unaweza kuvuta hisia za vijana barani Afrika, bila kujali mataifa wanayotoka. Tunayo furaha kubwa kuwa wadau muhimu katika kutambua, kukuza na hata kuboresha hazina hii kubwa ya muziki na utamaduni kutoka sehemu zote barani Afrika”.
Wanamuziki wanaoshindania tuzo hizi za MTV Africa Music Awards 2010 na kudhaminiwa na Zain walipendekezwa na MAMA Academy na kasha kuchaguliwa na timu ya wataalamu wa tasnia ya Muziki pamoja na wadau kutoka Afrika nzima. Washindi wa tozo ya MAMA 2010 watapatikana na kukabidhiwa tuzo zao katika ukumbi maarufu wa Eko Expo Center, jijini Lagos, Nigeria tarehe 11 Disemba mwaka huu.
0 Comments