Akizungumza na waandishi wa habari katika mkutano uliofanyika kwenye Hoteli ya Holiday Inn Jijini Dar es Salaam , Mwisho amekiri kuwa hana kinyongo na ushindi wa aliyekuwa rafiki na mshindani wake katika jumba Uti kutoka nchini Nigeria.
“Sina kinyongo na ushindi wa Uti kwani sisi kundi letu wote tumeibuka washindi isipokuwa Munyaradzi aliyekuwa akiwakilisha nchi ya Zimbabwe kwa kufika hatua ya fainali lakini fedha zilikuwa lazima apate mtu mmoja tu” anasema.
Aliongeza kwa kubainisha kwamba yeye na mshindi huyo ni marafiki na wamekuwa wakiwasiliana hata kabla ya mkutano huo kuanza huku akiwa amepokea zawadi kama Kamera pamoja na Laptop kutoka kwa Uti.
Akizungumzia vitu alivyovikosa wakati akiwa katika jumba lile alisema ni Kamusi ya lugha ya Kiswahili, vitabu ambavyo vinaonyesha ramani ya Tanzania na vivutio vyake ambavyo vingemsaidia kuwathibitishia wenzake kwamba Mlima wa Kilimanjaro uko Tanzania kwani hadi hivi sasa wapo ambao wanaamini kuwa mlina huo uko nchini Kenya.
Kutokana na kuwa yeye amejikita zaidi katika masuala ya Utalii akiwa anaishi Mkoani Morogoro Mwisho ameiomba Serikali kujitangaza zaidi kiutalii, madini na vivutio mbalimbali ambavyo viko nchini huku akisema ni jambo la kusikitisha kuona madini ya Tanzanite yanapatikana Afrika ambapo ni nchi ya Tanzania pekee ndipo yanapochimbwa lakini Bodi yake iko nchini Afrika Kusini.
“Hatujinadi kiutalii, nawashauri Bodi ya Utalii pamoja na Wizara ya Maliasili waunganishe nguvu wajitangaze katika vyombo vikubwa vya habari kama CNN nina hakika serikali ikiamua itaweza kwani siku zote biashara ni matangazo” alisema.
Wakati huohuo Mwisho amesema pamoja na kwamba hakuweza kuibuka mshindi katika shindano hilo anachojivunia ni kupata uzoefu ambao utamsaidia katika maisha yake ya kila siku.
0 Comments