- NBAA YATOA MSAADA KWA WATOTO 200 HOSPITALI YA RUFAA YA MKOA MOROGORO  - WATOTO 200, WASIOJIWEZA 25 WAPATIWA MSAADA WA DAWA NA MATIBABU MOROGORO - NBAA  BODI ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA) imetoa msaada wa dawa za dharura pamoja na vifaa mbalimbali katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro, kwa lengo la kuwasaidia watoto wadogo wasiopungua 200 wanaopatiwa huduma kila siku hospitalini hapo, ikiwemo dawa za watoto, pampers, neti, sabuni za kufulia, water dispenser pamoja na kuchangia chupa 22 za damu.  Akiongoza zoezi la kukabidhi msaada huo, Mkoani Morogoro Mkurugenzi Mtendaji wa NBAA, CPA Prof. Siasa Mzenzi, amesema taasisi hiyo imeona umuhimu wa kusaidia hospitali hiyo kutokana na uhitaji mkubwa wa vifaa muhimu kama Dawa, neti na sabuni, ili kupunguza changamoto zinazowakabili wagonjwa.  Ameongeza kuwa msaada huo umetolewa wakati wa mafunzo kwa wahasibu yanayofanyika mkoani Morogoro, na kusisitiza kuwa ni vyema kwa wataalamu kutumia fursa kama hizo kuwasaidia wenye uhitaji, hususani wagonjwa na watoto, ili kuwasaidia kurejea katika afya njema na kuhakikisha watoto wanapata makuzi bora.  Mbali na msaada wa vifaa, wanachama wa NBAA wanaoshiriki mafunzo hayo wamechanga fedha zilizotumika kulipia gharama za vipimo na dawa kwa wagonjwa 25 wasiojiweza wanaopatiwa matibabu katika hospitali hiyo, hatua iliyolenga kupunguza mzigo wa gharama kwa wagonjwa hao.  Kwa upande wake, Dkt. Azael Kyando, amepokea msaada huo kwa niaba ya Mganga Mfawidhi na kuishukuru NBAA kwa msaada huo na kutoa wito kwa wadau wengine kujitolea kwa moyo ili kusaidia jamii, kuwa juhudi hizo huleta faraja kubwa kwa wagonjwa na kuchangia ustawi wa jamii kwa ujumla.