MAKAMU WA RAIS DKT. NCHIMBI AFUNGUA DAKHALIA YA SKULI YA SEKONDARI YA HASNUU MAKAME KATIKA SHAMRASHAMRA ZA TAMASHA LA KIZIMKAZI

  

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi amesema Serikali itaendelea kutenga rasilimali za kutosha ili kuhakikisha skuli zote zinakuwa na miundombinu ya kisasa, walimu wenye sifa, na vifaa stahiki vya kufundishia na kujifunzia.

Makamu wa Rais amesema hayo, wakati wa hafla ya Ufunguzi wa Jengo la Dakhalia katika Skuli ya Sekondari ya Hasnuu Makame iliyopo Kibuteni Unguja, Zanzibar, ikiwa ni shamrashamra ya Tamasha la Kizimkazi (Kizimkazi Festival 2026). Amesema jitihada za Serikali katika kuimarisha miundombinu ya elimu ni endelevu ambazo zinajumuisha upatikanaji wa vifaa vya kufundishia, samani na upatikanaji wa walimu wenye sifa.

Makamu wa Rais amesema lengo la uwekezaji huo, ni kuandaa vijana wenye maarifa, ubunifu na ujuzi utakao wawezesha kujitegemea na kuchangia kikamilifu katika ujenzi wa Taifa. Amewasihi kutunza Dakhali hiyo na miundombinu mingine ya elimu kwa umakini mkubwa. Ametoa rai kwa Wananchi, Wazazi na walezi wa eneo hilo kuunga mkono jitihada za Serikali kwa kuwahimiza vijana kusoma kwa bidi na kulinda miundombinu ya elimu ya eneo hilo.
Aidha, Makamu wa Rais amesema mageuzi makubwa yaliyofanyika katika sekta ya elimu Zanzibar na Tanzania kwa ujumla yamekuwa na matokeo mengi chanya, ikiwemo kuongezeka kwa idadi ya wanafunzi wanaoandikishwa katika ngazi mbalimbali za elimu, kuimarika kwa miundombinu ya ufundishaji na ujifunzaji, ambako kumesababisha kuongezeka kwa ufaulu wa wanafunzi katika mitihani ya kitaifa.
Amesema Dakhalia hiyo iliyofunguliwa ni sehemu ya miradi lukuki inayotekelezwa Zanzibar yenye lengo la kukuza na kuendeleza sekta ya elimu na kuifanya kuwa ya mfano wa kuigwa kupitia uwekezaji mkubwa katika sekta ya elimu, na miundombinu ya kisasa kote.

Vilevile, Makamu wa Rais amesema ufunguzi wa dakhalia hiyo unakwenda kutatua moja ya changamoto kubwa iliyokuwa inawakabili wanafunzi ya kutembea umbali mrefu na kutumia muda mwingi kwenda na kurudi skuli. Pia mazingira mazuri yanayotokana na kuwepo kwa dakhalia hiyo yataongeza umakini, nidhamu, na ushirikiano wa karibu miongoni mwa wanafunzi, ambapo pia ni fursa nzuri kwa walimu kuwasimamia, kuwalea, na kuwasaidia kikamilifu katika masomo yao ya kila siku. visiwani.

Kwa upande wake Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Serikali ya Mapinduzi, Zanzibar Mhe. Lela Mussa amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, imeendelea juhudi za kuboresha elimu ikiwemo kusudio la kuondoa utaratibu wa wanafunzi kusoma katika awamu mbili yaani mchana na jioni ambao umekuwa ukiwaathiri katika elimu zingine ikiwemo masuala ya kidini.

Amesema uwekezaji wa Serikali ya Awamu ya Nane katika elimu unajidhihirisha wazi ambapo bajeti ya elimu imetoka bilioni 256 hadi kufikia trilioni 1.1 ikiwa ni uwekezaji mkubwa wa serikali kuhakikisha inaweka mazingira wezeshi ya kutekeleza malengo endelevu ya dunia katika nyanja ya elimu.

 

Imetolewa na

Ofisi ya Makamu wa Rais

11 Agosti 2026

Zanzibar.

Post a Comment

0 Comments