Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimesema Uongozi katika ngwe ya pili chini ya Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi utaiachia Zanzibar alama zisizofutika kwa maendeleo ya nchi na watu wake.
Alama na zawadi hizo zitabaki kuwa kumbukumbu za kudumu za maendeleo ya Zanzibar.
Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, Idara ya itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis, ameeleza hayo mbele ya waaandishi wa habari ofisi kwake Kisiwandui Mjini Unguja.
Katika maelezo yake, Mbeto alitaja ujenzi wa uwanja wa Ndege wa kisasa huko Pemba na barabara ya lami ya njia nne toka Chake Chake hadi Mkoani yenye urefu wa lilomita 45.3 mkoa wa Kusini Pemba.
Kadhalika Mbeto alisema utafanyika ujenzi wa Kijiji cha Michuano ya Soka ya Mataifa ya Afrika (AFCON) ambapo uwanja mkubwa wenye uwezo wa kuchukua zaidi ya washabiki 40 unajengwa Fumba, Mkoa wa Mjini Magharibi.
Pia akataja ujenzi wa barabara toka Tunguu-Makunduchi hadi Kizimkazi Mkoa wa Kusini Unguja yenye urefu wa kilomita 47.
"Sera za CCM chini ya SMZ katika uongozi wa Rais Dkt. Mwinyi utaacha alama za kudumu. Alama hizo zitabaki kuwa kumbukumbu muhimu kwa maendeleo ya waZanzibari wote " alisema Mbeto.
Akiitaja miradi mingine, alisema ni ujenzi wa bandari ya abiria huko Maruhubi kwa Mpigaduri na ujenzi wa nyumba za makazi ya wananchi zaidi ya 10,000 Unguja na Pemba.
"Kutakuwa na usafiri wa mfumo wa mabasi ya kisasa ya abiria na watalii katika Mji wa Unguja. Pia zitajengwa treni zitakazopita kwenye barabara za lami. Ujenzi wa barabara ya lami inayounganisha Mkoa wa Mjini na Kaskazini Unguja toka Kinazini hadi Bububu " alieleza mwenezi huyo.
Akifafanua zaidi, alisema kuna mradi wa uzalishaji wa umeme utakaomaliiza kero hiyo kwa Zanzibar, hospitali ya kufundishia ya kisasa na Chuo Kikuu cha Afya kitakachojengwa Binguni Mkoa wa Kusini Unguja.
"Serikalii chini ya Utawala wa Rais Dkt. Mwinyi utaacha alama zisizofutika Unguja na Pemba. Atakapoondoka madarakani atakumbukwa kwa kuitumikia nchi na watu wake" alieleza Mbeto.

0 Comments