GUTERRES: TANZANIA NI ‘MFANO WA AMANI DUNIANI ’


"Tanzania inaendelea kuwa mfano wa amani na mshikamano wa kijamii barani Afrika na duniani kote."

Hayo ni maneno ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Mheshimiwa António Guterres, alipokuwa akipokea ujumbe maalumu kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo.

Ujumbe huo uliwasilishwa na Mjumbe Maalum, Mheshimiwa Balozi Mahmoud Kombo, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Katibu Mkuu Guterres alitambua kuwa sifa ya Tanzania kama nembo ya amani ilipimwa wakati wa Uchaguzi Mkuu uliofanyika tarehe 29 Oktoba 2025. Hata hivyo, alipongeza uthabiti wa nchi katika kudumisha umoja na utulivu wa kitaifa.

Alisisitiza ni maslahi ya Umoja wa Mataifa kuiona Tanzania ikiendelea kubaki imara na kutumika kama mfano chanya.

Katibu Mkuu huyo wa UN pia alisisitiza umuhimu wa mazungumzo ya kitaifa yenye maana na jumuishi. Lengo la mazungumzo hayo ni kushughulikia mizizi ya matukio ya vurugu yaliyotokea tarehe 29 Oktoba 2025, na kuweka mikakati ya kuzuia kujirudia kwa matukio kama hayo.

Alihitimisha kwa kuthibitisha msaada kamili wa Umoja wa Mataifa kwa jitihada zinazoendelea za Tanzania, ikiwemo kutoa msaada wakati na baada ya kukamilika kwa kazi ya Tume ya Uchunguzi iliyoanzishwa nchini humo.

Post a Comment

0 Comments