MBETO: WATALII WAFURIKA ZANZIBAR


Na Mwandishi Wetu, Zanzibar

Miji ya Unguja na Pemba Zanzibar imefurika watalii wanaokuja kuvinjari katika fukwe namba tatu kwa ubora Duniani, kipindi hiki cha Sikukuu za Krismas na Mwaka Mpya 2026 tofauti na propaganda kuwa watalii wameikimbia Zanzibar kufuatia uhalifu uliofanywa na makundi ya vijana waliotumiwa na watu wenye nia ovu dhidi ya uchumi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania baada ya uchaguzi mkuu 29 Oktoba 2025.

Akizungumza Mjini Unguja, Zanzibar Katibu wa Kamati Maalum ya NEC, Zanzibar Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo Khamis Mbeto Khamis alisema, kuanzia Mjimkongwe, Paje hadi Jambiani takriban hoteli zote zimejaa.

Alisema madai ya kukimbia watalii hazina ukweli na baadhi ya wadau waliulizia kwenye mitandao lakini elimu na ufafanuzi kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, balozi za nje nchini, Mawakala na Kamisheni ya Utalii Zanzibar kuwa hali ni shwari na salama kumefanya wapuuze uzushi huo na kuendelea kumiminika Zanzibar.

"Zanzibar imefurika watalii sina pa kuwaweka" alisema na kuongeza kuwa mwishoni mwa wiki katika Uwanja wa Ndege wa Abeid Amaam Karume wamepokeaa ndege iliyobeba watalii zaidi ya 160 kutoka Hispania na nyingine toka Italia.

Alisema watalii hao mara nyingi wakitoka Zanzibar huelekea katika Hifadhi za wanyamapori Tanzania Bara, huenda wakaongezeka maradufu kufuatia vijana kukataa kutumika katika maandamano ya uharibifu wa mali yaliyokuwa yakihamasishwa kufanyika jana 09 Desemba 2025.

Mbeto alisema maandamano hayo ambayo kimsingi ni vita vya kiuchumi yalilenga kuvuruga amani na utulivu hivyo kukwamisha jitihada za kimaendeleo zinazofanyika.

Post a Comment

0 Comments