Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
Mpango uliopo wa kidunia hivi sasa ni kuhamasisha vurugu na uharibifu wa miundombinu ili kuhakikisha vyama vya ukombozi Afrika vinang’oka madarakani.
Akizungumza na wanahabari Ofisi Kuu ya CCM, Kisiwandui 30 Novemba 2025, Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis alisema mpango huo ndio ambao umeviondoa vyama kadhaa vya ukombozi, madarakani.
Mwenezi Mbeto anavitaja vyama hivyo kuwa ni pamoja na KANU (Kenya), UNIP (Zambia), MCP (Malawi) na vingine ambavyo viling’olewa kwa hila kutokana na kuonekana kuwa kikwazo kwa wenye malengo yao binafsi.
Alisema kilichotokea Tanzania Bara ni mwendelezo wa huo mpango ambao unatokana na wivu wa mipango ya maendeleo hususan iliyopo katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025-2050.
Alisema upanuzi na ujenzi wa bandari ya Tanga, Bagamoyo, Mtwara, Dar es Salaam na zilizopo Ziwa Tanganyika, Victoria, Nyasa sanjari na ujenzi wa reli ya kisasa ya treni za mizigo ni kati ya fursa ambazo zinataka kuvurugwa.
Mbeto alisema Bandari ya Mtwara inaboreshwa, serikali ipo katika mipango ya kujenga reli ya kisasa ya SGR kwa treni ya mizigo ambayo itatoka bandarini hapo hadi Ziwa Nyasa na kuhudumia nchi za Malawi, Zambia na Msumbiji” alisema.
“Rais Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi wametengeza miundombinu mizuri kulingana na Ilani ya CCM, lakini hivi karibuni tumeshuhudia uharibifu mkubwa Bara” alisema.
Alisema baada ya miaka 10 hadi 15 Tanzania inaenda kuwa ndio nchi ya kwanza Afrika yenye miundombinu ya kisasa inayoweza kuunganisha bara zima na Dira 2050 ni kuhudumia Ukanda wote.
Alisema nchi yoyote inayotaka maendeleo ni lazima kuwekeza katika miundombinu mizuri, bora na ya kisasa ili kuvutia utalii na uwekezaji kitu ambacho kinafanywa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na Rais Dkt. Mwinyi kwa Zanzibar.
Alisema Rais Dkt. Mwinyi kaiunganisha Zanzibar yote kwa miundombinu ya barabara za kisasa zenye taa na njia za waenda kwa miguu, madaraja na barabara za Juu Flyover.
“Barabara za juu eneo la Mwanakwerekwe zimeanza kutumika na zingine zinajengwa eneo la Amaani na hivi sasa nchi nzima vikiwemo visiwa vinaunganishwa kwa miundombinu ya barabara, vivuko na madaraja” alisema.
Mbeto alisema kuwa miundombinu yote hiyo inastahili kutunzwa na kutokana na yaliyotekelezwa awamu iliyopita ya sasa 2025/2030 inaenda kuifanya Zanzibar kuwa katika viwango vingine kabisa.
“Nimesafiri nchi mbili tatu unakuta katika mji kuna usafiri wa umma zaidi ya wa aina tano kuna subway, under ground, mwendokasi, treni za umeme, teksi na hicho ndicho kinachoenda kutokea Zanzibar ndani ya miaka mitano ijayo ya Dkt. Hussein Ali Mwinyi” alisema.
Mbeto alibainisha Ujenzi wa paa la tatu (Terminal III) la uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Amani Abeid Karume umefikia asilimia 80 achilia mbali miundombinu ya stendi, masoko ya kisasa vitu ambavyo ni sehemu ndogo ya kubwa ya ujenzi wa miundombinu ili kurahisisha shughuli za uzalishaji na kuvutia utalii na uwekezaji.
Mbeto analitaja Bandari Jumuishi ya Mangapwani ambayo itakuwa na uwezo wa kuhudumia meli kubwa za mizigo kutoka Mataifa mbalimbali ulimwenguni badala ya kuwa kama ilivyo sasa ambapo, zinatia nanga bandari za nje ya Zanzibar kisha mizigo kuletwa na meli zingine ndogo.
Zanzibar na Tanzania Bara alisema itakuwa sehemu kubwa ya biashara na hiyo ndio maana kinachotokea kinaitwa vita ya kiuchumi.
Mwenezi huyo, amewasihi waTanzania kwa ujumla wake kutambua kuwa kinachojengwa sio mali ya serikali wala CCM ni ya wananchi, hivyo wasije kujaribu kuiharibu.
“ Ni utekelezaji mzuri wa Ilani iliyopita na mwanzo wa mpya ya 2025-2030 na tunaendelea kuimarisha miundombinu ili iweze kurahisisha uchumi wa Zanzibar’’ alisema.
.jpg)
0 Comments