Ithibati ya waandishi wa habari imeendelea kujidhihirisha kama nguzo muhimu ya ulinzi wa Taifa katika dunia ya sasa inayotawaliwa na vita ya taarifa.
Kupitia Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB), inayotoa ithibati na vitambulisho vya uandishi wa habari kwa waandishi wenye vigezo kwa mujibu wa Sheria ya Huduma za Habari, Taifa linapata waandishi wanaotambulika, wanaowajibika na wanaofanya kazi kwa kufuata misingi ya taaluma, weledi na maadili.
Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Bw. Greyson Msigwa, wakati akizungumza katika kikao kazi na waandishi wa habari kilichoratibiwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) tarehe 18 Desemba 2025 jijini Dar es Salaam.
Amesema kuwa hatua hiyo inasaidia kudhibiti upotoshaji wa taarifa na kulinda taswira ya nchi ndani na nje ya mipaka yake kwani dunia ya sasa haipigani tena vita kwa silaha za kijeshi pekee, bali kwa taarifa zinazozalishwa na kusambazwa kupitia mitandao ya kijamii.
Amesisitiza kuwa katika mazingira hayo, waandishi waliothibitishwa wanakuwa mstari wa mbele kulinda usalama wa Taifa kupitia taarifa sahihi, zenye weledi na uzalendo.
Msigwa ameongeza kuwa kipindi kigumu kilichopita kimeonesha wazi jinsi taarifa potofu zinavyoweza kuchochea taharuki na kuathiri mshikamano wa kijamii.
Hata hivyo, amepongeza waandishi wa habari wa Tanzania, hususan wazalishaji wa maudhui mtandaoni, kwa kuonesha uzalendo na nidhamu ya taaluma kwa kutokutumia kalamu zao vibaya, licha ya shinikizo kubwa la mitandao na madai ya nje kwamba waandishi wa Tanzania ni dhaifu.
Kwa mujibu wa Msemaji Mkuu wa Serikali, ithibati si kikwazo cha uhuru wa habari bali ni nyenzo ya kulinda taaluma na waandishi wenyewe. Waandishi waliothibitishwa wanatambulika rasmi kama wadau wa ulinzi wa Taifa na taarifa wanazozalisha zinakuwa silaha ya kulinda amani, umoja na uthabiti wa nchi badala ya kuchochea migawanyiko.
#ithibatitz
#ithibatikidijitali



0 Comments