Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimewataka vijana Kanda ya Afrika Mashariki na Kati kuzipenda, kuzilinda na kuziepusha nchi zao kuziingiza kwenye kadhia ya mivutano na mizozo isiyo na ulazima wowote.
Pia chama hicho kimewahimiza vijana, kutofuata mkumbo na ushawishi wenye taaswira ya nguvu ya ukoloni na kuridhia kupoteza uhuru, utu na thamani ya kujitawala.
Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis ameeleza hayo katika mahojiano maalum na wanahabari, Zanzibar 02 Desemba 2025 kuhusiana na mustakbari wa vijana ktk siasa na kuwahimiza kujali maslahi ya nchi zao.
Mbeto aliitaja mivutano, mabishano na mizozo si njia sahihi ya kufikia utatuzi wa changamoto zinazojitokeza isipokuwa njia sahihi ni mazungumzo yatakayopelekea maridhiano.
Alisema vyombo vya Ulinzi na Usalama katika nchi zote ulimwenguni huapa kulinda mipaka, usalama wa raia wake na mali zao, hivyo si vyema kwa vyombo hivyo kulazimishwa kuingizwa kwenye mizozo.
" Kazi za vyombo vya dola zimetajwa kisheria na kikatiba za nchi zote. Hivyo si rahisi vikakwepa kutii dhamana hizo na kutojilinda lilipotokea tishio la hujuma au vurugu dhidi ya amani" alisema Mbeto.
Aidha aliwaasa vijana kutojiona wana jukumu la kuyapenda, kuyalinda na kuyatetea mataifa yao dhidi ya njama zozote kwani nje ya Afrika Mashariki vijana hao hawana mahali pa kwenda kuishi" alieleza.
Katibu huyo Mwenezi alisema waasisi wa Mataifa hayo wametumia nguvu nyingi, jasho na muda wao hadi baadhi yao kufa kwa kupigania uhuru wa nchi zao kwa kuwa kazi ya kuleta uhuru haikuwa nyepesi.
"Bila vijana kuwa na tahadhari watajikuta wakikwepa kubeba uzalendo hivyo kizazi cha sasa kinaweza kuingia katika historia isio na heshima kufuata mkumbo jambo ambalo si fahari kwao" alisema.
Mwenezi huyo alisema wakoloni hawajawahi kuwa na nia njema na Afrika licha ya kurudi katika nchi zao, kwani mara zote hulitamani Bara hili na kutaka kulipangia masharti ya hovyo.
"Vijana wa Afrika Mashariki na kati amkeni na kataeni kutumiwa na kuzirudisha nyuma kimaendeleo nchi zenu" alisema Mbeto.

0 Comments