CCM YAONYA WATEULE MIUNDOMBINU ZANZIBAR


Na Mwandishi Wetu, Zanzibar

Chama  Cha Mapinduzi (CCM), kimesema hakitamvumilia mteule yeyote wa Rais wa Awamu ya Nane, Dkt. Hussein Ali Mwinyi wala taasisi yoyote itakayoshindwa kusimamia utunzaji wa miundombinu ya  kisasa  inayojengwa  Zanzibar kwa ajili ya maendeleo ya wananchi.

Akitoa tathmini   ya ziara inayoendelea ya Rais Dkt. Mwinyi  ya uzinduzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku ya Mapinduzi ya Zanzibar, Katibu wa  Kamati Maalum NEC, Zanzibar Idara  ya  Itikadi,Uenezi na Mafunzo Khamis Mbeto Khamis  alisema  kote walipoenda katika ziara hiyo, Rais Dkt. Hussein Mwinyi anasisitiza utunzaji miundombinu.

"CCM tunaunga mkono kauli yake na tunafuatilia  na tunasisitiza kuwa hatutamvumilia mteule  au mtendaji yeyote atakaye zembea kwenye eneo lake na kushindwa kuitunza, kuilinda miundombinu hiyo dhidi ya uharibifu ukiwemo wa makusudi na itaishauri serikali kuchukuliwa hatua mtu yeyote yule aliyepewa dhamana akashindwa kuitekeleza na kusababisha uharibifu.

Alibainisha kuwa miundombinu hiyo imejengwa kwa gharama kubwa na kodi za  wananchi ili iweze kudumu kwa muda mrefu na kuendelea kutoa tija tarajiwa inatakiwa kutunzwa na kulindwa na CCM  haipo tayari kwenda kuadhibiwa na wananchi kwa wateule waliopewa dhamana  kushindwa  kuisimamia na kuifanya iharibike baada ya muda mfupi.

Aliitaja miundombinu hiyo ni ile  ambayo imejengwa na serikali katika kila sekta zikiwemo barabara, hospitali, vituo vya àfya na vifaa vyote vilivvyofungwa kwa ajili ya  uchunguzi wa afya, shule za kisasa za msingi na sekondari zenye vifaa vyote muhimu kwa ajili elimu bora kwa watoto kulingana na vigezo vya Kimataifa ya ufundishaji na Nyumba za Maendelep zilizojengwa kwa ajili ya wananchi na kuzinduliwa hivi karibuni na  Rais Dkt. Mwinyi.

Mbeto akigusia suala la elimu  kufuatia uzinduzi wa Shule ya Msingi Muungano yenye ghorofa tatu, madarasa 42 , vyoo 52, chumba cha Tehama, Maabara na Maktaba, huko Kibandamaiti 27 Desemba 2025, Mbeto alisema hadi itakapomalizika 2026 hakuna shule itakayokuwa na mikondo miwili ya kuingia darasani.

Alisema Zanzibar katika elimu inafuata vigezo vya Kimataifa kulingana Shirika la Umoja wa Mataifa la Sayansi, Elimu na Utamaduni (UNESCO) ya kutaka wanafunzi wasizidi 45 darasani, ubora wa elimu na mahitaji yote muhimu na mazingira mazuri ya kufundishia na kujifunzia.

"Tunafuata vigezo  vya Umoja wa Mataifa katika elimu" alisema Mwenezi Mbeto na kuongeza kuwa maslahi na ajira kwa walimu serikali inatekeleza ikiwa ni maagizo ya Ilani na Sera ya CCM kuhusu elimu..

Post a Comment

0 Comments