MBETO: WABUNGE, WAWAKILISHI ACT WAZALENDO MKAMSAIDIE DKT. MWINYI



Na Mwandishi Wetu, Zanzibar

Wabunge na Wawakilishi wa Chama cha òACT Wazalendo waliopata ridhaa ya wananchi na kuingia katika Baraza la Wawakilishi, wametakiwa wakaitumikie Zanzibar na sio vyama vyao ili kuchangia mandeleo makubwa zaidi katika kazi nzuri iliyoanzishwa na Rais Dkt. Hussein Mwinyi.

Akizungumza na wanahabari, ofisi za CCM Zanzibar, Katibu wa Kamati Maalum ya NEC, Zanzibar, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo Khamis Mbeto Khamis alisema uchaguzi umepita na ACT Wazalendo wameshinda Majimbo 10 kati ya 50 ya Zanzibar na wamepata Viti Maalum vinne vya Ubunge hivyo wakawe wawakilishi wema wa wananchi waliowachagua kwa ustawi wa Zanzibar ijayo.

"Wakaisimamie vizuri serikali ya Umoja wa Kitaifa, waihoji vizuri kuhusu ahadi yake kwa wananchi waliowachagua, waungane na wenzao wa CCM kwa ajili ya waZanzibari sio vyama vyao" alisema Mbeto.

Alibainisha kuwa wabunge na wawakilishi hao wa ACT Wazalendo kati yao wengine wanaweza kupata uwaziri katika Serikali ya Mapinduzi (SMZ) na pia Rais ana viti vyake 10 vya uteuzi ubunge, hivyo lolote zaidi linaweza kutokea kwani Zanzibar ni ya waZanzibari wote.

Mwenezi Mbeto alisema chama chake kinawapongeza ACT na vyama vingine vilivyoshiriki uchaguzi kwa amani na CCM ipo tayari kukaa meza moja na kujadili lolote lile linalohusiana na maendeleo na ustawi za Zanzibar na wananchi wake.

Kulingana na mabadiliko ya 10 ya Katiba ya Zanzibar ambayo yanasimamia uundwaji wa serikali ya umoja wa Kitaifa, chama cha pili katika matokeo ya kura ambacho kitapata asilimia 10 ya kura zote kinatoa Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar.

Kutokana na ACT Wazalendo kupata asilimia 23 ya kura zote katika uchaguzi wa 29 Oktoba 2025, kitatoa majina matatu kwenda kwa Rais wa Zanzibar ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi ambaye atateua mojawapo na kulitangaza ndani ya siku saba kwa mujibu wa katiba na ndilo tukio linalosubiriwa kwa hamu kubwa na waZanzibari hivi sasa.

Katika uchaguzi huo, mgombea wa CCM, Rais Dkt. Hussein Mwinyi aliibuka na ushindi mkubwa katika historia ya mfumo wa uchaguzi wa vyama vingi kwa siasa Zanzibar kwa kupata asilimia 74.8.

 

Post a Comment

0 Comments