DKT. MWINYI: TUJIFUNZE YALIYOTOKEA BARA 

Na  Mwandishi Wetu, Zanzibar

Wananchi wa Zanzibar wametahadharishwa kujiepusha na mambo yanayochangia uvunjifu wa amani kwani ikitoweka hakuna ambaye anaweza kufanya chochote na hata Ibada hazitaweza kufanyika.

Akizungumza wakati wa Dua Maalum ya Kuliombea Taifa na kushukuru na kuiombea amani iliyopo Zanzibar, iliyofanyika Masjid Jaamui Zinjibar, Mazizini leo 28 Novemba 2025, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Husseim Ali Mwinyi alisema Taifa linapaswa kujifunza  kwa yaliyotokea Bara.

Alisema kilichotokea hakikutegemewa na awali kilikuwa kinaonwa katika mataifa mengine na haikufikiriwa kama ingetokea Tanzania Bara.

"Tulikuwa tunaona kwenye tv mambo kama hayo yakitokea kwa wenzetu Libya, Yemen, Syria..., leo tumeyaona Bara na yanaweza kufika kwetu (Zanzibar), tutunze amani yetu" alisema.

Alibainisha kuwa ilivyotokea hivyo upande wa Bara, imesemwa na mwakilishi wa Sheikh Mkuu wa Baraza Kuu la Waislamu (BAKWATA), Sheikh Nuhu Mruma katika dua hiyo kuwa hata Ibada ya Ijumaa ilizuiwa na kila mmoja alitakiwa kuswali nyumbani kwake.


"Hilo liwe fundisho kwetu, amani ikiwa hakuna hakuna kinachoweza kufanyika na kilichotekea huko kinaweza pia kutokea Zanzibar hivyo ni wajibu kila mmoja kuitunza amani iliyopo.

Alisema vurugu hizo zimekuwa pia na athari za kiuchumi na kijamii kwani bidhaa hazikuweza kuingia Zanzibar na wananchi pia wapo walioguswa na vurugu hizo kwani Zanzibar na Bara zinategemeana.

Rais Dkt. Mwinyi alisema kuna watu walio katika makundi matatu ambao wanawajibu wa kuchunga sana matamko yao.

Aliwataja  wanasiasa kwa kuwa wanawafuasi wanaowasikiliza, viongozi wa dini wanaoaminiwa na waumini wao na wanahabari kwani jambo likiandikwa linaaminiwa na wananchi walio wengi.

"Leo ukiwaambia watu watoke, unategemea nini? Kama kuna tatizo lolote tukae tuzungumze" alisema na kuongeza kuwa Zanzibar waliomba amani wakati wa daftari la wapiga, kura, uandikishaji, upigaji kura, kuhesabu na hata wakati wa kutangazwa matokeo.

"Mwenyezi Mungu ametusaidia kwa mara ya kwanza uchaguzi umefanyika kwa amani, tudumishe amani na tuiombee Bara amani yao iweze kurudi na tujihadhari na mitandao ya jamii kwani inahubiri vurugu, iwe fundisho, Mungu azidi kudumisha amani yetu" alisema Rais Dkt. Mwinyi.

Awali akizungumza katika dua hiyo, Katibu Mtendaji Ofisi ya Mufti Zanzibar Sheikh Khalid Ali Mfaume aliwashukuru viongozi wa dini zote, wananchi, serikalì na wanasiasa ambao walihimiza kutunza amani ya Zanzibar na kutakiwa kuendelea kuiombea idumu na kuiombea Tanzania Bara iwe na amani.

Aliwataka vijana waliopo nje waache kuitukana nchi yao na wajipambe kwa tabia njema sio uharibifu ili wapate umri zaidi wa kuishi na hifadhi.

Post a Comment

0 Comments