TUNGUU ,MAKUNDUCHI KUWA NJIA NNE

Na Mwandishi Wetu, Zanzibar

mbea wa nafasi ya Rais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema serikali inakusudia kukamilisha ujenzi wa barabara ya njia nne ya Tunguu hadi Makunduchi pamoja na barabara za ndani Katika Mkoa wa Kusini Unguja.

Rais Dkt Mwinyi ameyasema hayo leo tarehe 16 Oktoba 2025 alipozungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika uwanja wa michezo wa Paje, Mkoa wa Kusini Unguja.

Mradi mwingine ameutaja kuwa ni ujenzi wa madaraja kwa ajili ya kuiunganisha mikoa ya Kusini na Kaskazini Unguja kwa ujenzi wa daraja la Unguja Ukuu- Uzi Ng'ambwa unaoendelea pamoja na wa daraja la Chwaka hadi Charawe.

Dkt. Mwinyi amewahakikishia wananchi ujenzi wa bandari ya Kizimkazi pamoja na kuziimarisha bandari ndogo za Mtene, Chwaka na Unguja Ukuu na wa kiwanja cha ndege cha Nungwi na kiwanja cha Paje na kuelezea kuwa kukamilika kwa miradi hiyo kutaufungua mkoa wa Kusini kiuchumi na ustawi wa jamii.

Rais Dkt. Mwinyi alisema serikali itajenga madarasa mapya katika mkoa wa kusini ikiwemo madarasa 1000 kwa shule za msingi na mengine 1000 kwa za Sekondari utakaombatana na shule za msingi nne na kumi za sekondari zote zikiwa za ghorofa.

Kuhusu sekta ya afya alisema serikali inajipanga kujenga hospitali ya mkoa wa Kusini Unguja wakati tayari ikiendelea na ujenzi wa Hosptali ya Rufaa ya kufundishia ya Binguni na Hospitali Kutibu Saratani ya Binguni na kuhusiana na suala la maji ameeleza kuwa serikali inajipanga kutekeleza mradi mkubwa wa maji katika mkoa huo utakaogharimu Dola za Marekani Milioni 55, Mradi utakaomaliza tatizo la Maji Mkoani humo.

Ameyataja maeneo yatakayonufaika na mradi huo kuwa ni Uroa, Marumbi, Pongwe, Jambiani na Makunduchi.

Eneo jingine ni kuwawezesha wanachi kiuchumi kwa kuwapatia mafunzo, vifaa vya kutendea kazi, mikopo isio na riba na kuwawekea mazingira bora ya kufanyia kazi zao kwa wajasiriamali.  

Rais Dkt. Mwinyi ameendeleza kuwahimiza wananchi umuhimu wa kudumisha amani wakati huu kuelekea Uchaguzi na baada ya uchaguzi kwani ndio nyenzo muhimu ilioiwezesha serikali kutekeleza miradi mingi ya maendeleo katika miaka minne iliopita.


 Mgombea huyo wa CCM kwa nafasi ya Rais wa Zanzibar amewaomba wananchi kumchagua tena kuiongoza Zanzibar ili aendelee kuleta maendeleo makubwa zaidi chini ya Kaulimbiu yake ya "Yajayo ni neema zaidi'.

Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi Zanzibar Dkt, Muhammed Said Dimwa amemuelezea Dkt. Mwinyi kuwa kiongozi muadilifu, mkweli na mwenye hekima katika utendaji wake na kuwaomba wananchi kumchagua tena kuiongoza Zanzibar kwa mafanikio zaidi.

Post a Comment

0 Comments