RC KUNENGE APIGA KURA AHIMIZA WANANCHI WENGI KUSHIRIKI UCHAGUZI LEO

 

Mkuu wa Mkoa wa Pwani  Abubakari Kunenge akitekeleza  zoezi la kupiga kura leo asubuhi aliposhiriki katika kituo chake  kilichopo Wilayani Kibaha.

Na Mwandishi Wetu, Pwani

Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhe. Abubakari Kunenge, ametoa wito kwa wananchi wote wa mkoa huo kuendelea kujitokeza kwa wingi kushiriki katika zoezi hilo muhimu la kidemokrasia, akisisitiza kuwa kufanya hivyo ni haki yao ya kikatiba.

Kunenge ametoa wito huo leo Oktoba 29, 2025 mara baada ya kushiriki kupiga kura mapema asubuhi ya saa moja kwenye kituo cha Ofisi ya mkuu wa Mkoa katika uchaguzi mkuu unaofanyika kote nchini, ambapo Watanzania wanawachagua viongozi watakaoongoza kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.

Akizungumza mara baada ya kupiga kura, Mh. Kunenge alisema Mkoa wa Pwani upo shwari, ulinzi umeimarishwa, hivyo kila mtu ana uhuru na usalama wa kutimiza wajibu wake wa kikatiba na akaishukuru Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi kwa maandalizi mazuri yaliyowezesha zoezi la upigaji kura kuendelea kwa utulivu na kwa mazingira rafiki kwa wapiga kura.

“Kama mnavyoona, vituo vya kupigia kura vimewekwa karibu na vipo vya kutosha ili kuepusha msongamano wa watu na kuondoa usumbufu wa wapiga kura kusafiri umbali mrefu,” alisema Kunenge.

Aidha, alieleza kuwa utaratibu wa kupiga kura ni rahisi na hauchukui muda mwingi, akibainisha kuwa karatasi za kura zimeandaliwa kwa ufasaha zikiwa na picha za wagombea pamoja na alama za vyama husika, hivyo kumpa mpiga kura urahisi wa kufanya maamuzi.

Post a Comment

0 Comments