Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
Mufti Mkuu wa Zanzibar, Sheikh Saleh Omary Kabi amebainisha kuwa uchaguzi ni jambo la hakika na haki kulingana na makubaliano ya masheikh, ulamaa na wanazuoni wa Zanzibar, waliokutana kabla ya mapinduzi ya mwaka 1964.
Akizungumza na waumini wa dini ya kiislamu mara baada ya Ijumaa iliyofanyika Masjid Jamii, Zinjibar Mazizini, Unguja, Zanzibar leo 25 Oktoba 2025 ambako Rais wa Zanzibar ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi na anagombea nafasi ya Rais wa Zanzibar katika uchaguzi ujao 29 Oktoba 2025 alikuwepo kwa ibada, Muft Mkuu Kabi, alisema jopo hilo la wanazuoni lilithibitisha hilo na pia imeandikwa katika kitabu kitakatifu cha waislam.
Alisema Zanzibar sio mara ya kwanza kufanya uchaguzi wa vyama vingi vya siasa na uchaguzi wa kwanza ilikuwa 1963.
Kutokana na hali hiyo amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi wakiwa na furaha kwenda kupiga kura kwa amani na kurudi nyumbani.
"Hata kitabu kitakatifu kinaeleza kuwa uchaguzi ni jambo la haki" alisema na kuongeza kuwa wagombea pia pepo ipo upande wao watapokuwa na subira na kushukuru kulingana na matokeo.
Alibainisha kuwa atakayeshinda, akashukuru kwa Mwenyezi Mungu milango ya pepo inakuwa wazi na atakayeshindwa akahuzunika, akawa na subira na kushukuru kwa matokeo hayo atalipwa bila hesabu kesho ahera.
"Mungu atamlipa mema mengi mazuri aliyeshindwa na kuwa na subira kisha akashukuru.
Katika ibada hiyo ambayo ilimjumuisha pia Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Hemed Suleiman Abdullah, alisema uchaguzi ni Ibada na ukihuzunika leo, kesho utafurahi ili mradi ukishindwa usibeze wala ukishinda usifanye dhihaka.
Awali akitoa mawaidha wakati wa sala hiyo ya Ijumaa, Katibu Mtendaji, Ofisi ya Mufti Mkuu Zanzibar, Sheikh Khalid Mfaume alisema imeandikwa kwamba lazima mmoja aongoze wenzake hata watu wakiwa wawili.
"Wote hatuwezi kuwa viongozi ni lazima mmoja aongoze na pia tumeagizwa kuzitii mamlaka" alisema.

0 Comments