Kuunganishiwa umeme hivi sasa Zanzibar ni TSh. 100,000 badala ya 200,000 bila mwananchi kutozwa gharama za nguzo ikiwa ni ahadi ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, wakati akiwania Urais katika uchaguzi mkuu uliopita, 2020.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Mradi wa Maboresho ya Umeme Zanzibar, uliofanyika Verde, Mtoni Unguja, alisema kukamilika kwa mradi huo kumefanya hivi sasa kumalizika kwa changamoto ya umeme mdogo na kukatika katika na kuwezesha kupokea megawati zote 132 kutoka gridi ya Taifa badala ya 114 zilizokuwa zinafika na zingine kupotea.
Mradi huo ambao umegharimu Dola za Marekani, Milioni 8.4 umetekezwa kwa wakati na kampuni ya Novavis ya waZanzibari (Diaspola), wanaoishi Marekani na kina kazi ya kuchuja umeme unaopokelewa, kudhibiti mgandamizo na kiwango cha umeme unaoingia.
"Kulikuwa na malalamiko mengi hasa kutoka kwa wawekezaji
kwenye mahoteli kuwa umeme mdogo" alisema na kuongeza kuwa hilo sasa limeisha na miradi ya umeme katika vyanzo tofauti inaendelea kutekelezwa lengo ni Zanzibar kujitosheleza kwa umeme wake yenyewe tena wa uhakika.
Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Nishati na Madini Zanzibar, Joseph Kilangi alisema kuna miradi ya nishati inatekelezwa ikiwa ni pamoja na umeme jua, kutumia nguvu za nyuklia, upepo na vyanzo vingine kutokana na uwekezaji unaofanyika kuhitaji kiwango kikubwa cha umeme tofauti hata na ilivyo sasa.




0 Comments