Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
Mgombea wa nafasi ya Rais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ameeleza kuridhishwa na hali ya ufanyaji biashara katika eneo la Darajani.
Ameeleza kuwa lengo la Serikali ni kuliimarisha eneo hilo na kuendelea kujenga zaidi ili wafanyabiashara wapate maeneo mazuri ya kufanyia biashara.Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo alipokutana na wafanyabiashara na wajasiriamali wa soko la Darajani, akiwa katika mfululizo wa kampeni zake za kuomba kura na kuzungumza na makundi mbalimbali ya wananchi.
Amesema kuwa eneo jingine ni ujenzi wa maegesho katika eneo la Malindi, ili kuondoa utaratibu wa kuegesha magari kiholela, na kueleza kuwa mradi mkubwa wa BIG Z, utakaojenga maduka pembezoni mwa barabara, unakuja na utaongeza haiba ya eneo la mjini.
Akizungumzia barabara ya Malindi hadi Mnazi Mmoja, amesema itatengenezwa na kufanyiwa upanuzi kuwa ya njia nne, pamoja na ujenzi wa maegesho katika eneo la Malindi.
Rais Dkt. Mwinyi amesema kuwa katika awamu ijayo, Serikali inakusudia kuongeza fungu la fedha kwa ajili ya utoaji wa mikopo kwa wafanyabiashara na wajasiriamali, hususan wale waliokopa awali na kurejesha fedha kwa wakati.
Kuhusiana na kodi, amesema Serikali itakaa na CCM ambacho ndicho chombo kinachohusika na masuala ya sera, ili kulipatia ufumbuzi suala hilo na kuona uwezekano wa kupunguza kodi.
Ameliagiza Shirika la Umeme (ZECO) kuweka transfoma mpya katika eneo hilo ili kumaliza tatizo la umeme.
Wakiwasilisha risala yao, wafanyabiashara wa Darajani Souk wameeleza kunufaika na mageuzi makubwa yaliyofanyika katika eneo hilo ikiwemo mazingira bora ya kufanyia biashara, kurudishwa kwa kituo cha daladala na kuboreshewa bustani, mambo yaliyoongeza idadi ya wanunuzi.




0 Comments