Na Mwandishi Wetu Zanzibar
Mgombea wa nafasi ya Rais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema Chama Cha Mapinduzi kitaendelea kuhubiri amani na umoja, na hakuna mtu atakayebaguliwa kutokana na asili yake.
Amewahakikishia wananchi kuwa asili ya mtu si kigezo cha kubaguliwa, na kwamba Chama Cha Mapinduzi kinawatambua wananchi wote kuwa Wazanzibari na si vinginevyo.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo, tarehe 15 Oktoba 2025, alipokutana na makundi ya wajane, wafuasi wa imani ya Rastafarian, jamii ya Wahindu na Ismailia katika mwendelezo wa kampeni zake za kukutana na makundi mbalimbali ndani ya jamii, hafla iliyofanyika Ukumbi wa Idrissa Abdulwakil, Kikwajuni, Mkoa wa Mjini Magharibi.
Ameyanasihi makundi hayo kuendelea kukiamini Chama Cha Mapinduzi kwa kuwa ndicho chama pekee kinachohubiri na kulinda amani ya nchi wakati wote.
Rais Dkt. Mwinyi amewahakikishia wajane kuwa Serikali inaandaa sheria kali dhidi ya wazazi wanaotelekeza watoto wao, na kwamba hatua madhubuti zitachukuliwa katika awamu ijayo kwani malezi bora ni haki ya msingi ya mtoto.
Ameongeza kuwa hakuna kundi litakaloachwa katika mpango wa uwezeshaji, ambapo katika awamu ijayo Serikali inajipanga kuyafikia makundi yote ambayo bado hayajafikiwa ili kuyapatia mikopo nafuu yatakayoyasaidia kujikwamua na umaskini.
Aidha, Rais Dkt. Mwinyi ametoa wito kwa makundi hayo kujitokeza kwa wingi siku ya kupiga kura tarehe 29 Oktoba mwaka huu, na kuwahakikishia kuwa amani ya kutosha itakuwepo ili uchaguzi ufanyike kwa salama, amani na utulivu.
Wakizungumza katika mkutano huo, wawakilishi wa makundi hayo wamempongeza Rais Dkt. Mwinyi kwa kuwathamini, kuwaleta pamoja na kuwajumuisha katika kampeni zake, na wamemuahidi ushirikiano pamoja na kumpa kura ili aendelee kuiongoza Zanzibar kwa ajili ya kuleta maendeleo zaidi.




0 Comments