DKT. MWINYI :SERIKALII ITAJENGA MAENEO MENGI ZAIDI YA WAJASIRIAMALI Z'BAR

Mgombea wa nafasi ya Rais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema Serikali itahakikisha inatengeneza maeneo mengi zaidi ili wajasiriamali wafanye biashara zao kwa utulivu na mazingira bora zaidi.


Ameeleza kuwa Serikali inaendelea kufanya kila juhudi kuhakikisha inazipatia suluhisho changamoto zinazowakabili wajasiriamali, ambao wengi wao ni wanawake.

Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo tarehe 09 Septemba 2025, alipokutana na makundi ya wajasiriamali katika Ukumbi wa Idrisa Abdulwakil, Kikwajuni, Mkoa wa Mjini Magharibi, katika mwendelezo wa kampeni zake za kuzungumza na makundi mbalimbali ya wananchi.

Kuhusiana na mafunzo, amewataka Wakala wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Zanzibar (ZEEA) kutoa mafunzo kwa wajasiriamali kabla ya kuwapatia fedha za mikopo, ili fedha hizo ziwanufaishe na ziwasaidie kufikia malengo yao.

Ameeleza kuwa Serikali ilitenga shilingi bilioni 96 kwa ajili ya kuwawezesha wajasiriamali nchini, lakini baadhi yao hawakufikiwa, hivyo Serikali imejipanga kuja na utaratibu bora zaidi utakaowafikia wale waliokosa fursa hiyo awali.

Rais Dkt. Mwinyi amewahakikishia wajasiriamali kuwa Serikali itawafikia katika maeneo yao na kuwapatia mikopo midogo midogo ili kuwainua kiuchumi na kupunguza changamoto za maisha.

Aidha, ameeleza kuwa Serikali itaendelea kutenga fedha za kutosha kwa ajili ya kutoa mitaji kwa wajasiriamali na ameahidi kuweka utaratibu mzuri zaidi wa kuhakikisha fedha hizo zinawafikia walengwa.


Akizungumzia suala la masoko, amesema Serikali itajipanga na kuzungumza na wawekezaji ili kuweka utaratibu maalum wa kuwatafutia masoko ya bidhaa zao, hususan katika hoteli za kitalii.

Kuhusu viwanda vidogo, amesema Serikali itatenga fedha kwa ajili ya kuanzisha viwanda vidogo vidogo vitakavyowaajiri wananchi wengi zaidi, sambamba na kurahisisha upatikanaji wa mikopo kwa wajasiriamali.


 Amefahamisha pia kuwa mradi mkubwa wa BIG Z unalenga kujenga vibanda bora vya biashara pembezoni mwa barabara za mjini kwa ajili ya wajasiriamali kufanya biashara zao katika mazingira salama na ya kisasa.

Rais Dkt. Mwinyi ametumia fursa hiyo kuwaomba wajasiriamali kujitokeza kwa wingi kupiga kura na kumchagua kwa kura nyingi pamoja na wagombea wengine wa CCM, ili aweze kuiongoza tena Zanzibar kwa awamu ya pili na kuleta maendeleo makubwa zaidi.

Post a Comment

0 Comments