Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo imefafanua kuhusu taarifa zilizosambaa mitandaoni zikionyesha wachezaji wa Pamba Jiji FC wakifanya mazoezi gizani katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa taarifa ya Wizara, timu hiyo ilifika uwanjani hapo jana majira ya saa 12:35 jioni bila kutoa taarifa rasmi ya kufanya mazoezi ya kujiandaa na mchezo wao dhidi ya Yanga SC unaotarajiwa kuchezwa kesho, Septemba 24, 2025.
Kutokana na kutokuwepo kwa taarifa mapema, wataalamu wa umeme walikuwa tayari wameondoka, na ilibidi warudishwe kazini. Taa za uwanja ziliwashwa majira ya saa 1:08 usiku.
Wizara imesikitishwa na kusambazwa kwa picha zilizoonyesha wachezaji wakifanya mazoezi gizani, ikibainisha kuwa chanzo cha hali hiyo ni uzembe wa Pamba Jiji FC yenyewe. Aidha, imeeleza kuwa kitendo hicho kimeathiri taswira ya menejimenti ya uwanja, ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikizingatia taratibu zilizowekwa.
Kwa msingi huo, Wizara imezitaka timu zote zinazotumia Uwanja wa Benjamin Mkapa kuzingatia masharti na kutoa taarifa mapema kabla ya kufanya mazoezi ya mwisho, ili kuepusha sintofahamu zisizo za lazima.

0 Comments