Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
Mikopo kwa ajili ya boti kubwa za uvuvi ipo mbioni kuanza kutolewa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa wavuvi wa Unguja na Pemba.
Akizungumza akiwa Unguja, Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo Khamis Mbeto Khamis alisema boti hizo ni mbali ya zingine 1500 za kisasa zenye vifaa vyote muhimu, zilizotolewa kwa wavuvi na wakulima wa mwani.
Mbeto alisema boti hizo kubwa za uvuvi za kisasa zitawawezesha wavuvi kufika kina kikubwa cha bahari hivyo kupata samaki wa wengi na kwa uhakika.
Alisema boti hizo wamekabidhiwa zikiwa na jaketi za usalama, rada na kifaa maalum cha kubaini samaki walipo.
"Hivi sasa husikii habari za kupotea wavuvi baharini maana wana rada inayowaongoza sio kama wakati ule wakitumia ngalawa" alisema Mbeto.
Pia wakulima wa mwani hivi sasa wanaenda maji kina badala ya ufukweni hivyo kupata mwani ulio bora sio uliochanganyika na takataka au mchanga.
Sanjari na hilo, ujenzi wa masoko ya samaki yenye vyumba vya baridi (Cold room) kwa ajili ya kuhifadhia umefanyika na iwapo Dkt. Mwinyi atachaguliwa tena, atajenga masoko zaidi ya namna hiyo.
Mbeto alitoa mfano wa soko la samaki Tumbe ambalo lina chumba cha baridi chenye uwezo wa kuhifadhi hadi tani 5,000 za samaki.
"Leo wakausha dagaa wa Ndagoni, Tama na Fungurefu hawaaniki dagaa juani kutwa nzima au hadi siku mbili, wanaweka kwenye mashine baada ya muda mfupi wanawatoa na kuwaingiza sokoni, nani anasema eti Dkt. Mwinyi anashughulika na miradi mikubwa na sio maisha ya watu?" alihoji Mbeto.


0 Comments