Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani leo limeendesha mafunzo ya siku moja kwa waandishi wa habari wa Mkoani hapa yanayohusu Wajibu na Usalama wa Waandishi wa Habari wakati wa uchaguzi 2025.
Akizungumza na waandishi hao kwenye mafunzo yaliyofanyika kwenye Ukumbi wa mikutano uliopo kwenye jengo la Polisi Mkoa wa Pwani RPC Salim Morcace amewasisitiza wana habari kuchakata taarifa zenye tija, weledi na uzalendo kwa sababu vyombo vya habari wanalo jukumu la kulinda amani ya nchi.
"Wajibu wa Jeshi la Polisi katika kulinda usalama wakati wa uchaguzi uwepo wa Jeshi la Polisi Tanzania ni kwa mujibu wa sheria mama yaani katiba ibara ya 147(4), Kuhusu uundwaji /uanzishwaji wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama" amesema RPC Morcace.
"Jeshi la polisi lina jukumu la kulinda maisha na mali za wananchi kubaini ,kuzuia na kutanzua uhalifu,kupeleleza,kuhifadhi ushahidi na kukamata" amesisitiza RPC Morcace.
Akiwasilisha mada hiyo Kamanda Morcase amewasisitiza Waandishi wa Habari Mkoa wa Pwani kuweka mbele maslahi ya umma ikiwa ni pamoja na kuandika habari kwa kutanguliza uzalendo katika kulinda na kuendeleza ustawi wa umma.
SSP Elias Haway ametoa rai kwa Waandishi kuepuka kubashiri matokeo ya uchaguzi, kueneza taarifa za uvumi ,kupendelea na kuripoti madai yasiyothibitishwa ama yaliyochakatwa makusudi kwa nia ovu kwa kutumia teknolojia ya kidigiti.
"Vyombo vya habari viepuke kurusha au kuchapisha matangazo ya kampeni ujumbe wa kumuunga mkono mgombea au kuchakata maudhui yoyote ya kisiasa yenye muelekeo wa kampeni kwenye magazeti ,redio, televisheni, na majukwaa ya kidigiti pale inapofikia ukomo wa kampeni kwa mujibu wa Tume Huru ya Uchaguzi INEC".
"Vyombo vya habari havitaruhusiwa kuwa na vituo vya kujumlisha matokeo na badala yake vitapaswa kuripoti matokeo rasmi ya uchaguzi kutoka kwenye Tume Huru ya Uchaguzi INEC amesema SSP Haway.
Aidha SSP Ibrahim Nkindwa amesisitiza Waandishi wazingatie usalama wao kwanza pamoja na wengine ambao ni wanajamii tupeane elimu lipi ndilo na lipi halistahili.
"Epukeni kupokea rushwa ili kuandika habari za kupendelea upande fulani kwani Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU wako kazini.
Wakati huohuo SSP Nemes Kavishe Mkuu wa Kikosi Cha Kutuliza Ghasia
Mkoa wa Pwani amesema kuwa anatoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi katika kushiriki Uchaguzi Mkuu ujao uliopangwa kufanyika tarehe 29, Oktoba 2025 kwa utulivu na amani sambamba na kutii sheria bila shuruti .
"Haki bila wajibu haviendi sambamba"amesema SSP Kavishe.
Mkaguzi wa Polisi Jesca Mwaikugile ambaye pia ni Afisa Habari wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani.
INSP Mwaikugile amesisitiza kuwa Jeshi hilo litaendelea kufanya kazi na Waandishi wa Habari ambao wataripoti habari za uchaguzi ni wale ambao wamepata Ithibati kutoka Bodi ya JAB ambao ni waandishi wa muda, waajiriwa wa kudumu na wanafunzi ambao wanafanya mafunzo kwa vitendo watakao pangiwa kazi kipindi cha uchaguzi.
ASP Mwaikugile amesisitiza waandishi kutovaa mavazi yenye kuashiria itikadi ya chama chochote cha siasa kwani ni kinyume na taaluma ya habari.
Mafunzo hayo yameshirikisha Waandishi wa Habari kutoka vyombo mbalimbali vya habari Mkoani Pwani.
Waandishi hao wameaswa kutoandika habari kwa mihemko ya ushabiki na shauku kupita kiasi ,kutokuandika habari ambayo haijakamilisha pande mbili zinazohusika ,kukwepa kuandika habari zenye upendeleo na kujikita kishabiki.




0 Comments