Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Jacob John Mkunda akimvisha cheo kipya Sajini Alphonce Simbu ambaye ni Mshindi wa Medali ya Dhahabu ya Marathon ya Dunia KM 42 kuwa Sajinitaji ofisini kwake Makao Makuu ya Jeshi Upanga, Dar es Salaam asubuhi leo tarehe 25 Septemba 2025.
Na Mwandishi Wetu,
Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Jacob John Mkunda amempongeza Sajini Alphonce Simbu kwa ushindi wa medali ya dhahabu katika Mashindano ya Mbio za Marathon ya Dunia kilomita 42 zilizofanyika Jijini Tokyo Japan.
Pamoja na pongezi hizo,
Jenerali Mkunda amempandisha cheo kutoka Sajini kuwa Sajinitaji tukio lililofanyika ofisini kwake Makao Makuu ya Jeshi Upanga Jijini Dar es Salaam tarehe 25 Septemba 2025.
Amesema ushindi huu ni kwa watanzania wote na Afrika kwa ujumla na kwamba michezo ni sehemu ya kazi jeshini hivyo Sajinitaji Alphonce Simbu amefanya kazi nzuri.
Jenerali Mkunda ametoa rai kwa Maafisa na Askari wote jeshini waige mfano wa Sajinitaji Simbu kwa kufanya kazi kwa bidii na kuleta mafanikio katika kila idara tofauti jeshini.
Naye, Mkuu wa Mafunzo na Operesheni wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania Meja Jenerali Ibrahim Mhona amesema safari hii katika michezo Jeshi limefanya vizuri sana ambapo tarehe 26 Septemba 2025 Katika Uwanja wa Golf Lugalo, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi atapokea vikombe kutoka timu za Jeshi zilizofanya vizuri katika Mashindano mbalimbali ndani na nje ya nchi, ikiwemo Mashindano ya Baraza la Michezo ya Majeshi Tanzania (BAMMATA), Mashindano ya Kombe la Mkuu wa Majeshi (CDF CUP) na Medali aliyoipata Sajinitaji Alphonce Simbu.
Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Jacob John Mkunda akizungumza na mshindi wa Medali ya ya Dhahabu ya Marathon ya Dunia Sajinitaji Alphonce Simbu Makao Makuu ya Jeshi Upanga, Dar es Salaam.Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Jacob John Mkunda akipokea Medali ya dhahabu kutoka kwa mshindi wa Mashindano ya Marathon ya Dunia Sajinitaji Alphonce Simbu ofisini kwake Upanga, Dar es salaam



0 Comments