PROF. JANABI AWAAGA WATUMISHI MUHIMBILI, ABAINISHA NAMNA RAIS SAMIA ALIVYORAHISISHA USHINDI WAKE

Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani kanda ya Afrika na Mkurugenzi Mtendaji Hospitali ya Taifa Muhimbili Prof. Mohamed Janabi amewaaga watumishi wa hospitali hiyo kupitia Mkutano wa 30 wa Baraza la Wafanyakazi liliofanyika katika Ukumbi wa PSSSF mkoani Dar es Salaam.

Prof. Janabi amewashukuru watumishi wote kwa ushirikiano waliompatia kipindi chote cha uongozi wake ambao umewezesha hospitali kupata mafanikio makubwa na kuendelea kuwa tumaini kwa huduma za afya ndani na nje ya nchi.

Prof. Janabi amewaomba watumishi hao kuendelea kufanya kazi kwa weledi, bidii na kujitoa zaidi ili mafanikio yaliyopatikana yaendelee  kuleta mageuzi makubwa katika utoaji wa huduma za afya katika ukanda wa Afrika Mashariki, kati na Kusini mwa Jangwa la Sahara.

“Siwezi kusema kuwa haya nimeyafanya mwenyewe, haya yamewezekana kwa kujitoa kwenu, kuwa waaaminifu na uzalendo mkubwa katika kuhakikisha kuwa tunatoa huduma hizi kwa wananchi kwa weledi na maarifa yanayohitajika” amebainisha Prof. Janabi

Prof. Janabi amewashauri watumishi wa hospitali kutokakata tamaa kuomba nafasi za kimatifa zinapojitokeza kwa kuwa hayo yote yanawezekana pale mtu atakapojiamini kuwa anaweza kutekeleza majukumu hayo.

Aidha, Prof. Janabi amemshukururu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kumpendekeza pamoja na namna alivyojenga mahusiano mazuri na mataifa mengine ya Afrika ambayo yamemuwezesha kupata nafasi hiyo barani Afrika.

Prof. Janabi aliteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuiongoza hospitali hiyo Oktoba, 2022 kuchukua nafasi ya aliyekuwa Mkurugenzi wa Hospitali hiyo Prof. Lawrence Museru baada ya kustaafu.

Post a Comment

0 Comments