MSAMA :VIONGOZI WA DINI MSIHUBIRI SIASA MADHABAHUNI

Muandaaji wa matamasha ya kidini ya Pasaka na Krismasi, Alex Msama, amewataka  viongozi wa dini nchini kuhakikisha kuwa nyumba za ibada zinabaki kuwa maeneo ya kuhubiri maadili, amani, na upendo — badala ya kuwa majukwaa ya mijadala ya kisiasa.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo  Juni 8 2025 Msama amesema kuwa ni muhimu kwa wachungaji na viongozi wote wa dini kuheshimu mamlaka zilizopo, kwa kuwa mamlaka hizo zimetajwa katika maandiko matakatifu kuwa zimewekwa na Mungu

“Huwezi kutumikia mabwana wawili kwa wakati mmoja,” amesema Msama. “Iwapo umechagua kuwa mtumishi wa Mungu, basi jitokeze wazi katika wito huo na uachane kabisa na siasa. Viongozi wa dini wanapaswa kuhubiri injili, kuwahimiza watu kuacha maovu na kumrudia Mungu, siyo kuchochea mijadala ya kisiasa.”

Msama amesema kuwa katika kitabu cha Warumi 13, maandiko yanasisitiza kuwa yeyote anayepinga mamlaka zilizowekwa, anapinga pia mpango wa Mungu.

“Maandiko yanasema wazi kuwa washindanao na mamlaka wanashindana na Mungu mwenyewe, si tu viongozi waliopo madarakani. Kwa hiyo si vyema kwa watumishi wa madhabahu kushiriki katika harakati au matamko yanayodhalilisha mamlaka halali,” amefafanua Msama.

Amesisitiza kuwa jukumu kubwa la  viongozi wa dini ni kuhakikisha taifa linadumu katika misingi ya upendo, mshikamano, na amani, kwa kutumia nafasi yao kuwahimiza waumini kuwa raia wema na watii wa sheria.

Post a Comment

0 Comments