📍 Aahidi Maboresho Makubwa Zaidi ya Miundombinu.
Na Mwandishi wetu, Tabora
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi leo Juni 23, 2025 amefanya ziara katika bustani ya wanyamapori ya Tabora maarufu kama 'Tabora ZOO' kwa lengo la kukagua na kuona usimamizi wa bustani hiyo ambapo ametumia fursa hiyo kuwahamasisha watanzania hususani wa ukanda wa magharibi, wakazi wa Mkoa wa Tabora na Mikoa ya jirani kutembelea kivutio hicho cha kipekee ambacho kipo Katikati ya Mkoa wa Tabora.
Katika ziara hiyo Dkt. Abbasi ameonesha kuridhishwa na uwepo wa bustani hiyo ambayo ni hazina ya vivutio vya wanyamapori na mazingira asilia.
Ameeleza kuwa Tabora ZOO ni sehemu muhimu ya utalii wa ndani ambayo serikali imejipanga kuhakikisha inafanya maboresho makubwa ya miundombinu ili kuvutia watalii wengi zaidi.
Aidha, Katibu Mkuu huyo ameahidi kuwa Serikali itaendelea kuboresha bustani hiyo kwa kuongeza miundombinu ikiwemo sehemu za watalii kupumzika na burudani kama michezo ya watoto, maeneo ya chakula, vinywaji pamoja na kuongeza Idadi ya wanyamapori na mabwawa ya maji ili kuongeza mvuto zaidi kwa watalii.
Katika ziara hiyo Dkt. Abbasi aliweza kujionea huduma mbalimbali zinazotolewa na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania - TAWA kupitia bustani hiyo ya wanyamapori na maendelezo yaliyofanyika ikiwemo ujenzi wa kituo cha maelezo Kwa wageni (VIC,), mabanda ya wanyamapori, ongezeko la wanyamapori wakiwemo simba, chui, duma, fisi na wengine wa aina mbalimbali.
Tabora ZOO ambayo ni mojawapo ya bustani chache za wanyamapori nchini zilizopo katika maeneo ya miji imeendelea kuwa kivutio cha kipekee Kwa watalii kutokana na mandhari nzuri na mazingira tulivu ambavyo vinaiweka bustani hii katika nafasi ya juu Kwa utalii wa mijini (Urban Wildlife Tourism).







0 Comments