Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amefanya ukaguzi wa Uwanja wa Shirika la Elimu Kibaha Mkoani Pwani ambapo utatumiwa kufanyia sherehe za kuwasha Mwenge wa Uhuru na kusema ameridhishwa na maandalizi aliyoyaona ikiwa ni ,jukwaa kuu mzunguko na watoto watakaocheza halaiki.
Waziri Mkuu amesema hayo leo tarehe 30 Machi 2025 alipofika kukagua maendeleo ya maandalizi ya Uwanja huo kwa ajili ya sherehe za kuwasha Mwenge wa Uhuru zitakazofanyika tarehe 2 Aprili 2025 ambapo ameonesha shauku ya kuuboresha zaidi Uwanja huo ili ukidhi vigezo vya timu zitakazoshiriki katika Michuano ya CHAN 2025 na AFCON 2027.
"Jana nimefanya ukaguzi Shirikisho la Mpira Tanzania (TFF) kufanya tathmini ya kazi ya ujenzi na ukarabati wa viwanja vya mazoezi vitakavyotumika kwenye michuano ya CHAN na AFCON viwanja ni vichache ila baada ya kufika hapa nimeridhishwa na hali ya Uwanja huu kwani una kidhi vigezo vyote vya kuleta timu zije kufanya mazoezi na hata mechi za Ligi Kuu Bara zinaweza kuchezwa katika Uwanja huu wa Shirika la Elimu Kibaha"
"Changamoto kubwa niliyoiona ni sehemu ya kuchezea (pitch) hii tutaitengeneza kwa kufukia madimbwi na kuusawazisha Uwanja , vyumba ya wachezaji (dressing rooms) pia ikumbukwe timu ikija kukufanya mazoezi Kibaha wachezaji watalala kwenye Hoteli za hapa hivyo tutaingiza fedha za kigeni.
Tayari Waziri Mkuu Majaliwa amekagua viwanja vya Gymkhana, Meja Generali Isamunyo na kiwanja cha Chuo cha Sheria(Law School ) kilichopo Simu 2000 Ubungo Jijini Dar es Salaam.
Michuano ya CHAN 2025 inayoshirikisha wachezaji wa ndani inatarajiwa kufanyika kuanzia tarehe 2 hadi 30 Agosti 2025 baada ya kuahirishwa mwaka 2024, Vilevile michuano ya Afcon inatarajiwa kufanyika mwaka 2027.
Akizungumza kuhusu maandalizi ya uzinduzi wa kuwashwa Mwenge wa Uhuru ambayo yamefikia asilimia 96 huku Mgeni Rasmi atakuwa Makamu wa Rais Dkt Philip Isdor Mpango.
Wakati huohuo amewatembelea vijana wanaocheza halaiki na kuwaahidi vifaa vyote wanavyotumia wakati wa mazoezi na waalavyotumia siku ya kuwashwa kwa Mwenge wa Uhuru ni vya kwao na asitokee mtu wa kuwanyang'anya.
0 Comments