BANDA LA WIZARA YA MALIASILI NA UTALII LAVUTIA MAONESHO YA NANENANE DODOMA

Baadhi ya wananchi wakiangalia mubashara bidhaa mbalimbali katika banda la Wizara ya Maliasili na Utalii katika maonesho  ya nanenane  yanayoendelea katika viwanya vya Nzuguni Jijini Dodoma 




Na Kassim Nyaki, Dodoma.

Banda la Wizara ya Maliasili na utalii limeendelea kutembelewa na idadi kubwa ya wananchi katika maonesho ya nanenane Dodoma kutokana na uwepo wa programu mbalimbali za utalii mubashara kupitia wizara na taasisi zake.

Tangu maonesho hayo yalivyoanza tarehe 1/08/2024 hadi kufikia siku ya leo jumapili zaidi ya wananchi 4000 wametembelea banda la Wizara ya maliasili na utalii ambapo wanapata fursa ya kuona vivutio vya utalii moja kwa moja kutoka eneo la hifadhi ya Ngorongoro kupitia Ngorongoro live stream, programu za utalii kupitia Screen kubwa ya utangazaji kwenye magari ya TANAPA, kuona Wanyamapori hai walioko eneo la banda, uoneshaji wa shughuli za kiutamaduni kupitia gari la Makumbusho ya Taifa, elimu ya wanyamapori kutoka chuo cha Wanyamapori MWEKA, bidhaa za asili na kitamaduni katika banda la wajasiriamali mbalimbali wanaoishiriki maaonesho hayo. 

Vilevile makundi ya wananchi wanaotembelea banda hilo wanapata elimu kuhusu vivutio vya utalii vilivyopo nchini, gharama za kuingia hifadhini, fursa za uwekezaji katika maeneo ya hifadhi, shughuli za upandaji miti na utunzaji wa mazingira na kuelimishwa hatua za upigaji kura kwa vivutio vya utalii vilivyoingizwa katika kinyang’anyiro cha kuwania tuzo za mtandao wa worlds travel awards kwa mwaka 2024.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa kamati ya maandalizi kwa upande wa wizara ya maliasili na utalii Bw. Juvenile J. Mwambi ambae ni, Kaimu Mkurugenzi Msaidizi Kitengo cha Maendeleo ya Utalii, amesema Wizara inaendelea kutoa elimu ya masuala ya uhifadhi, utalii, maendeleo ya jamii ambapo wizara hiyo pamoja na kushiriki maonesho hayo kitaifa Dodoma pia pia inashiriki katika maonesho yanayofanyika kikanda katika mikoa ya Arusha, Mbeya, Tabora, Morogoro, Mwanza na Simiyu. 

“Uongozi wa wizara kwa kushirikiana na wadau wa utalii tutahakikisha kuwa tunatumia mbinu zote kuhamasisha utalii wa ndani ili wananchi wengi waendelee kutembea maeneo ya hifadhi zetu na tuweze tufikia malengo ya watalii milioni tano ifikapo mwaka 2025, pia yapo maeneo ya uwekezaji katika hifadhi zetu ambapo Wizara tunashiriki programu za makongamano mbalimbali katika maonesho haya ili kutangaza fursa hizo kwa wageni wanaotembelea maonesho haya ili wazijue” ameongeza Mwambi.

Maonesho ya nanenane kwa mwaka 2024 yaliyoanza tarehe 01 agosti yanaendelea hadi tarehe 08 agosti 2024 ambapo kauli mbiu ya mwaka huu ni "Chagua viongozi bora wa Serikali za mitaa kwa maendeleo endelevu ya Kilimo, mifugo na Utalii"

Post a Comment

0 Comments