Picha ya pamoja ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Maj. Gen. Gaudence S. Milanzi (wa tano kushoto) na baadhi ya washiriki wa maonesho ya Kimataifa ya Utalii ya ITB 2018 yanayoendelea Jijini Berlin nchini Ujerumani.
Na Mwandishi Wetu - Berlin, Ujerumani
.................................................................................
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Maj. Gen. Gaudence S. Milanzi ameongoza msafara wa Tanzania unaoshiriki katika Maonesho ya Kimataifa ya Utalii ya ITB 2018 yanayoendelea Jijini Berlin nchini Ujerumani.
Lengo la Maonesho hayo ni kutangaza fursa za utalii zilizopo nchini Tanzania katika masoko mbalimbali ya utalii barani Ulaya na duniani kote.
Sekta ya utalii inachangia wastani wa asilimia 25 ya fedha zote za kigeni zinazoingia nchini Tanzania na asilimia 17.5 ya pato la Taifa .
Maonesho hayo yalianza tarehe 7 mwezi huu na yanatarajiwa kufikia tamati keshokutwa tarehe 11 Machi, 2018. Ushiriki wa Tanzania katika maonesho hayo umehusisha Sekta ya Umma na Sekta Binafsi.
Washiriki kutoka sekta ya umma ni pamoja na Idara ya Utalii – Wizara ya Maliasili na Utalii, Bodi ya Utalii Tanzania, Shirika la Hifadhi za Taifa, Mamlaka ya Hifadhi Ngorongoro na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania.
Kwa upande wa Sekta Binafsi jumla ya kampuni 60 zimeshiriki maonyesho hayo ikiwemo Kampuni moja inayoshughulika na uratibu wa matukio (Events and Exhibitions management), Kampuni tatu zinazoshughulika na usafiri wa anga, Kampuni ishirini na saba zinazoshughulika na huduma za malazi (hoteli, loji na kambi za utalii), na Kampuni ishirini na tisa za Wakala wa biashara ya kusafirisha watalii.
Pamoja na shughuli za maonyesho hayo, Katibu Mkuu Milanzi amefanya pia mikutano kadhaa na wadau wa utalii na washirika wa maendeleo waliopo nchini Ujerumani.
Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Maj. Gen. Gaudence Milanzi (wa pili kulia) akijadili jambo na wadau walioshiriki maonesho hayo kutoka Tanzania. Kulia ni Mkurugenzi wa Idara ya Utalii TANAPA, Ibrahim Mussa.
0 Comments