Social Icons

Wednesday, August 31, 2016

SIRI KUFA KWA MUZIKI WA JAMHURI YA MUZIKI WA KONGO (DRC)

MUZIKI wa Jamhuri ya kidemokrasi ya Congo (DRC), hivi sasa unaonekana kupoteza dira na mwelekeo wake kutokana na wanamuziki wake wakongwe wengi kupoteza maisha huku vijana wakikimbilia muziki na soko la nchi za Magharibi. Ukiusikiliza na kuutazama muziki huo kwa sasa wengi wao wamepoteza mashabiki, jambo ambalo linashabihiana na maneno yanayozungumzwa kwamba vifo vya wanamuziki wakongwe ambao walitamba katika miaka ya 1960 , !970, 1980 hadi mwishoni mwa miaka ya 1990 na tamati yao ilijionyesha mwishoni mwa mwaka 2000. Utafiti uliofanywa na MwanaHabari mwishoni mwa mwaka jana, gwiji la muziki kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Koffi Olomide alitangaza rasmi kustaafu kazi hiyo. Mwishoni mwa mwaka huohuo ulimwengu wa bakulutu ulipata pigo jingine baada ya kufariki kwa gwiji lake Tabu Ley aliyezikwa jijini Kinshasa. Je nini hatma ya muziki wa Congo na majaaliwa yake ya baadaye? Hili ni swali gumu kujibika kirahisi lakini ni wajibu na haki ya wadau kujua hatma ya muziki wa DRC na majaaliwa yake ya baadaye kwa sababu maisha ni lazima yaendelee hata kama kutakuwa na pengo la magwiji hawa wawili. Kama hiyo haitoshi pia itakumbukwa mwaka huu wanamuziki kutoka DRC , walipatwa na pigo la ghafla baada ya aliyekuwa galacha na mwalimu wa waalimu wa muziki wa Kongo Papa Wemba alipofariki dunia akiwa jukwaani nchini Ivory Coast wakati akitumbuiza kwenye tamasha maalum baada ya kuanguka na kuzirai. Itakumbukwa mazishi ya gwiji huyo wa muiondoko ya Soukus Mwili wake uliwekwa ndani ya jeneza la rangi nyeupe lililokuwa limefunikwa bendera ya Jamhuri ya Congo, ulilazwa kwenye majengo ya Bunge ili wadau wa muziki, wanamuziki wenzake na watu wengine zaidi ya elfu kumi wafike kutoa heshima za mwisho. Viongozi wa serikali ya DRC walihudhuria mazishi hayo huku wawakilishi kutoka nchi jirani ya Congo Brazaville pia walihudhuria. Mkali mwingine kutoka DRC,Tabu Ley ‘Rochereau’ , alifariki na kuzikwa Desemba 9, mjini Kinshasa. Mwanamuziki huyu alifariki Novemba 2013 akiwa na umri wa miaka 76 wakati akipata matibabu nchini Ubelgiji. Wengi watamkumbuka Tabu Ley kwa muziki wake na kwa ‘talanta’ yake kwenye tungo na nyimbo zake zilizowagusa watu wengi barani Afrika. Mwanamuziki huyo ambaye pia alikuwa mwanasiasa, hakuwahi kupona tangu alipougua maradhi ya kiharusi mwaka 2008 na hali yake iliendelea kuwa mbaya hadi alipofariki Novemba 30. Alizaliwa mwaka 1937 katika kijiji kimoja kidogo Magharibi mwa mkoa wa Bandundu, na hapo ndipo nyota yake ilianza kung'aa katika fani ya muziki wa Rhumba mapema miaka ya 1960. Baadhi ya nyimbo alizoimba zilikuwa ‘Adios’ ‘Thethe’ na ‘Mokolo Nakokufa’ zilizosaidia katika kuupandisha chati muziki wa miondoko ya Rhumba na kutokea kujizolea mashabiki wengi pamoja na kupendwa sana. Katika enzi za uhai wake Tabu Ley alitamani sana kuwa Kiongozi hasa cheo cha Waziri wa Utamaduni katika serikali ya Laurent-Desire Kabila, lakini badala yake akawa Naibu Gavana wa Jiji la Kinshasa. Alikimbilia uhamishoni wakati wa utawala wa Rais Mobutu Sese Seko Kukungenga wa Zabanga kati ya mwaka 1965-1997, na mwaka mwaka 1990, serikali ya Mobutu ikapiga marufu album yake iliyokwenda kwa jina la ‘Trop, c'est trop’. Hivi ndivyo tulivyompoteza gwiji Tabu Ley, kwa upande mwingine Koffi amestaafu kupiga muziki wa kutengeneza albamu na atabakia kupiga muziki wa jukwaani ‘live music’. Kwa maana nyingine ni kwamba sisi tuliombali na upeo wa macho yake hatutaonja ama kuisikia ladha ya muziki wake tena kwa siku za hivi karibuni labda kama atabadilisha mawazo. Hapa naliona tatizo tena kubwa la kukosekana kwa gwiji huyu mwingine wa muziki barani Afrika. Hivi sasa wadau na mashabiki wa muziki hawaushabikii tena muziki wa kutengenezwa studio bali kama ni gitaa basi tulione likikung’utwa tukiwa jukwaani. Kama ni tumba basi vile vile siyo vibaya tukamuona mpigaji akichanganya vionjo ili kuleta ladha yake halisi. Koffi aliyekuwa akiishi kwa wakati fulani kwenye majiji ya Kinshasa na Paris, Ufaransa hivi sasa amepiga kambi ya kudumu Kinshasa na shughuli zake za kimuziki anaziendeleza akiwa jijini humo. Kwa maana nyingine ili upate burudani yake ni lazima uwe na mkwanja mrefu ili kumkodisha yeye na bendi yake ya Quartier Latin. Chanzo cha habari cha uhakika kilichozungumza na mwandishi wa habari hizi kutoka jijini Kinshasa kinatanabaisha kwamba Koffi hivi sasa amepiga kambi eneo linaloitwa Macampagne. Ni eneo wanaloishi watu wenye uwezo kifedha ‘mapedeshee’ kama wanavyoitwa nchini kwetu. Jirani yake kabisa ni mwanamuziki mwenzake ‘JB’ Mpiana. Kulikuwa na taarifa kwamba wanamuziki kadhaa maarufu wa DRC wamepigwa marufuku kukanyaga nchini Ufaransa akiwemo Koffi Olomide kutokana na sababu za kisiasa. Inaelezwa kwamba mwanamuziki Koffi ni mtu wa karibu wa Rais Joseph Kabila na mpinzani mkubwa wa Kabila ni Etienne Tshisekedi ambaye anakubalika mno nchini Ufaransa kuliko hata Kabila jambo linalosadikika kuwa ndilo lililochangia kupigwa marufuku kuendelea kufanya shughuli zake za muziki nchini Ufaransa. Koffi alikuwa haendi Ufaransa kwa sababu kwanza wanenguaji wake wa zamani hususani walioweka makazi barani Ulaya walikuwa wamemfungulia kesi ya kuwaweka kinyumba kwa lugha nyingine ni kwamba alikuwa amewafanya watumwa wa ngono. Pili lipo kundi la Wakongo waishio barani Ulaya wanajiita ‘Kombataa.’ Hawa ni wale wanaompinga Rais Kabila. Kwa kifupi ni wapinzani wa Rais Kabila na hawataki msanii yeyote wa kutoka DRC aimbe nyimbo za kumsifia Kabila hususani wakati wa kampeni. Pia zipo taarifa kwamba baadhi ya wanamuziki walitunga nyimbo za kumsifia Kabila akiwemo Koffi Olomide. Hawa inaelezwa waliwahi kumshughulikia msanii mkongwe wa kike Elizabeth Shalamwana. Huyu aliwahi kufanya ziara barani Ulaya na alikumbana na kipigo kikali kutoka kwa ‘makombataa’ Anti Kabila. Kitisho cha hawa jamaa inaelezwa inaweza ikawa ni sababu nyingine ya Koffi kusita kubakia barani Ulaya akifanya shughuli zake. Bado wadau na wafuatiliaji wa duru za muziki wa DRC wameshikwa na bumbuazi kwani ni ukweli usiopingika kwamba mapengo ya wataalamu hawa katika fani yameacha pengo kubwa katika ulimwengu wa muziki wenye asili ya Kiafrika ‘Congolise’ na Ulimwenguni kote kwa ujumla. Uchawi sababu kuu iliyopoteza ladha ya muziki wa DRC Inadawaiwa Muziki wenye asili ya DRC umepotea kutokana na kuchangiwa na wanamuziki wake kugubikwa na imani za kishirikina. Jambo hili halina ubishi kwamba ni kweli wanamuziki wa DRC wamekuwa wakiamini kuwa bila uchawi muziki hauwezekaniki. Jambo hili wameweza kulithibitisha wenyewe katika nyakati tofauti kwamba ‘Juju’ kwenye muziki wao ni lazima. Jambo ambalo linasemekana ndilo lililo zipoteza bendi mbalimbali kama vile Extra Musica, Wenge BCBG, Wenge El Paris, Wenge Maison Mere, ajali ya ndege iliyosababisha vifo kwa waliokuwa wanamuziki waliokuwa Luciana waliotamba na miondoko ya ‘Zipompapompa’. Wanamuziki wengine kutoka DRC ambao hawasikiki tena ni pamoja na aliyekuwa Malkia wa Mutwashi Tshala Muana, Yondo Sister, Le General Deffao,Kanda Bongo Man,Burkina Fasso, Mbilia Bel na wengineo ambao licha ya umri kuwatupa mkono imekosekana kizazi kilichoweza kuwarithi umahiri wao hadi sasa.

No comments:

 
 
Blogger Templates