(Picha/Habari na Benedict Liwenga-WHUSM)
Serikali
imekutana na kufanya mazungumzo na baadhi ya Viongozi wa Mashirikisho ya Filamu
nchini ikiwa ni sehemu ya kubaini changamoto mbalimbali zinazoyakabili
Mashirikisho hayo.
Akiongea
hivi karibuni jijini Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi Idara ya Maendeleo ya
Sanaa, Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Bi. Leah Kihimbi alisema
kwamba, Mashirikisho yanayounda Shirikisho la Filamu nchini hayanabudi
kushirikiana kwa karibu na Serikali ili kubaini changamoto na namna ya
kuzitatua kwa manufaa ya Wasanii na Taifa kwa ujumla.
Alieeleza
kuwa, Wasanii wanapaswa kuzingatia maadili wakati wanapofanya kazi zao za sanaa
ili waweze kujijengea heshima kwao, kwa jamii ambayo ndio mlaji wa kazi zao za
kisanaa na kwa Taifa kwa ujumla.
“Mnapofanya
kazi zenu za sanaa, jitahidini kufuata miiko ya kazi zenu, tumieni vipaji vyenu
vizuri kwa kufuata maadili ya Kitanzania, lakini pia jitahidini kuwainua wale
wasanii wanaochipukia ama wale wadogo ili waweze kuwa na hamasa ya kuendeleza
kazi zao za sanaa”, alisema, Bi. Kihimbi.
Bi.
Kihimbi aligusia suala la fursa ya kazi za sanaa inayodhaminiwa na Taasisi ya
British Council Tanzania na kuwataka wasanii kuchangamkia fursa hiyo kwa
kuhakikisha kuwa kila msanii au kikundi kinaandika Pendekezo (Proposal) kuhusu fursa hiyo ili kujiwekea nafasi
kubwa kwa wasanii wa Tanzania kushinda fursa hiyo na kuweza kupata fedha za
kuendesha kazi za sanaa kulingana na wazo lililobuniwa.
“Kuweni
wabunifu katika hii fursa ili mje na wazo zuri ambalo litawawezesha kushinda
hii fursa hasa hii ya nAnA (new
Arts new Audiences) kwani
inamhusu msanii mmoja mmoja au kikundi”, alisema, Bi. Kihimbi.
Aliongeza
kuwa, Serikali itajitahidi kutatua baadhi ya changamoto ambazo zinaonekana kuwa
kero kwa wasanii nchini ikiwemo suala la wizi wa kazi za sanaa (Piracy) ambalo kwa sasa tayari Waziri mwenye
dhamana katika Wizara hiyo, Mhe. Nape Nnauye ameonyesha mfano kwa kukamata DVDs
feki pamoja na mitambo ikiyotumika kudurufu kazi hizo za sanaa nchini.
Kwa
upande wake, Katibu wa Bodi ya Filamu Tanzania, Bi. Joyce Fissoo alisema kwamba
Bodi yake inashirikiana vema na wasanii nchini kwa kuzingatia Sheria za nchi
pasipo kumuonea msanii yeyote na kuwataka wasanii kote kuendeleza uhusiano huo
mzuri uliopo kwa manufaa yao na Taifa kwa ujumla.
Aidha,
aliwataka viongozi wa Shirikisho hilo la Sanaa kuendelea na utaratibu wa
kupeana taarifa kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu sanaa na kuwahimiza
wasanii kupenda kujiendeleza kielimu ili waweze kumudu soko huku akiwasisitiza
kuhakikisha kuwa kazi zao wanazotengeneza zinapata kibali cha Bodi kwa kuwekewa
madaraja na zinakuwa na stika halali ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ili
kuepusha uharamia wa kazi zao.
Naye
Rais wa Shirikisho la Filamu Tanzania, Bw. Simon Mwakifwamba ameiomba Serikali
kuendelea kushirikiana na Wasanii kwa karibu kwa kuzifanyia kazi baadhi ya
changamoto wanazokabiliana nazo na ikiwemo suala la uharakishaji wa Sera ya
Filamu kwani ndiyo kipaumbele chao cha kwanza, elimu ya namna ya kutengeneza
filamu bora, usambazaji wa kazi zao pamoja na adui yao mkubwa ambaye ni
uharamia wa kazi za sanaa.
Ameishukuru
Serikali kwa kuunda Sekta mpya ya Sanaa na kusema kuwa, Sekta hiyo itakuwa
Mkombozi kwao kwani wanajisikia fahari kutambuliwa na kuwa na kitengo chao cha
masuala ya kazi zao huku akiaahidi ushirikiano mzuri kwa sekta hiyo.
0 Comments