WAKATI usajili kwa watu wanaotaka kushiriki mbio ndefu za Uhuru, maarufu kama Uhuru Marathon, zinazotarajiwa kufanyika Desemba 7, mwaka huu jijini Dar es Salaam ukiendelea kwa kasi kubwa waandaaji wa mbio hizo wamezindua mpango wa kujenga kituo cha michezo eneo la msoga Mkoani Pwani.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana,
Katibu wa Kamati ya mbio hizo, Innocent Melleck alisema,kamati ya Uhuru
Marathon imeona umuhimu wa kuanzisha kituo hicho ambapo jumla ya shilingi
bil.4.8 zinatarajiwa kutumika katika kukamilisha mpango huo.
“Tunapenda kutangaza rasmi kwamba Uhuru Marathon imenunua
shamba eneo la Msoga Mkoani Pwani lenye ukubwa wa ekari 25 kwa lengo la kujenga
kituo kikubwa cha kukuza vipaji vya wanamichezo mbalimbali mkoani pwani eneo la
msoga na kitajulikana kwa jina la Jakaya Kikwete Uhuru Sports Accademy na jumla
ya michezo 11 itahusishwa katika mkakati huo.
Tunatarajia kumkabidhi mheshimiwa Rais Kikwete mpango huu
wenye lengo la kuleta mafanikio makubwa ya michezo nchini ambapo watoto wenye
vipaji watapata nafasi ya kusoma na kukuzwa katika utaratibu wa michezo na tunaamini
kuwa baada ya miaka mitano hadi kumi tutaweza kuanza kupata mafanikio.
Kituo hiki ndicho kituo pekee katika ukanda wan chi za
Afrika Mashariki na Kati ambapo jumla ya wanamichezo 2300 wataweza kuwa katika
mpango wa awali.
Tunatarajia kupata nguvu toka katika wahisani mbalimbali wa
ndani na nje ya nchi kwa kuwa wapo wanaohitaji kuona Tanzania ikipata mafanikio
kupitia michezo.
Wakati huo huo zaidi ya wakimbiaji 2700 wameshachukua fomu
kwaajili ya kushiriki mbio za mwaka huu huku malengo makuu yakiwa ni kuhitaji
kushirikisha zaidi ya wakimbiaji 15,000.
Vituo vitakavyokuwa vikiuza fomu za ushiriki ni Tripple
seven Mikocheni, Maduka ya TSN na Uchumi Supermarket, Uwanja wa Leaderds Club,Ofisi za RT
Taifa,Stendi kuu ya mabasi Moshi Mjini, Arusha pia kwa kutumia tovuti ya www.uhurumarathon.com
0 Comments