Warembo walioingia katika Tano Bora kwenye Shindano la Redd's Miss Tanzania 2014.
Redd's Miss Tanzania Soitti Mtemvu akiwa na baba yake mzazai Abbas Mtemvu Mbunge wa Temeke mara baada ya kutwaa taji hilo.
.
NA MWANDISHI WETU
MREMBO Sitti Abbas Mtemvu (23), kutoka Temeke, Jumamosi usiku
alitwaa taji la Redd’s Miss Tanzania 2014, baada ya kuibuka kidedea kwenye
fainali za shindano hilo lililofanyika katika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar
es Salaam.
Sitti ambaye ni mtoto wa Mbunge wa Temeke, Abbas
Mtemvu alitangazwa kuibuka kidedea kwenye shindano hilo na Mkurugenzi wa Lino
Investment Agents waandaaji wa shindano hilo, Hashim Lundenga na kuwabwaga
walimbwende wengine 29 walioshiriki shindano hilo na kurithi taji kutoka kwa Happiness
Watimanywa ambaye alitwaa taji hilo mwaka jana.
Katika shindano hilo lililoanza majira ya saa 4:00
usiku wa kuamkia jana, lilishuhudia warembo wote 30 wakitoa shoo kali ya
ufunguzi kabla ya kupita jukwaani wakiwa na mavazi ya kubuni, ufukweni na vazi
la usiku kabla ya kutangazwa kwa 15 bora, huku Sitti akionekana kuwa na sapoti
kubwa jukwaani.
Baada ya kutangazwa kwa 15 bora washiriki walioingia
tano bora walitangazwa na kila mmoja kuulizwa swali lake huku huku Sitti
akitumia lugha ya Kifaransa na Kiingereza kujibu swali aliloulizwa
Nafasi ya pili kwenye shindano hilo lililopambwa na
burudani kutoka kwa Vanessa Mdee na Ommy Dimpoz, ilikwenda kwa Lillian
Kamazima, huku mrembo wa Ilala Jihhan Dimachk akishika nafasi ya tatu, Dorice
Mollel na Nasreem Abdul walishika nafasi ya nne na tano.
Akizungumza
baada ya mwanaye kutangazwa mshindi wa Redd’s Miss Tanzania, Mtemvu alisema
kuwa anaamini Sitti ataendelea na masomo baada ya kumaliza masuala ya urembo kwa
sababu alimuahidi hivyo na pia aliongeza kudai kuwa Sitti anaweza kutumia taji
hilo kuendeleza taasisi ya Mtemvu Foundation ambayo inasaidia vijana
waliokwenye mazingira magumu.
Kwa upande wa wake Sitti alisema kuwa moja ya vitu
vilivyompa ushindi kwenye kinyanganyiro hicho ni uwezo wake wa kuzungumza lugha
tatu, huku akikiri kuwa upinzani ulikuwa mkali kwa sababu warembo wote walikuwa
na vigezo vya kushinda.
Mshindi wa shindano hilo anajinyakulia kitita cha
shilingi milioni 18 na kuiwakilisha Tanzania kwenye mashindano ya dunia, huku
mshindi wa pili akinyakua shilingi milioni 6, mshindi wa tatu milioni 4.2 na
washiriki wengine wanapata kifuta jasho cha shilingi laki 7 kila mmoja.
Khadija Kalili na Somoe Ng'itu tulikuwepo .
0 Comments