Watoto
mapacha kutoka wilayani Kyela mkoani Mbeya waliokuwa wamepelekwa na
serikali chini ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kufanyiwa upasuaji
mkubwa wa kuwatenganisha wakiwasili nchini Tanzania kutokea nchini India
walipokuwa wakipatiwa matibabu katika hospitali ya watoto ya Appolo.
Kulia ni Mkuu wa Kitengo cha Magonjwa ya Nje wa Wizara ya Afya na Ustawi
wa Jamii Dkt. Edward Sawe, mama mzazi wa watoto hao Bi. Grace Joel na
Daktari aliyekuwa akiwaangalia nchini India Dkt.Glory Joseph.
Watoto hao wakiwa wamebebwa na Daktari aliyekuwa akiwaangalia nchini India Dkt.Glory Joseph (kushoto) na mama mzazi wa watoto hao Bi. Grace Joel.
Mama mzazi wa watoto
hao Bi. Grace Joel akiwa amewabeba watoto wake Elikana Erick (kushoto)
ns Eliud Erick (kulia) mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa ndege wa
kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es salaam.
******************************
Picha na Stori Na. Aron Msigwa – MAELEZO
Hatimaye
watoto mapacha kutoka wilayani Kyela mkoani Mbeya waliokuwa wamepelekwa
na serikali chini ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kufanyiwa
upasuaji mkubwa wa kuwatenganisha jana jioni wamerejea nchini wakitokea
nchini India katika hospitali ya watoto ya Appolo walikokuwa wanapatiwa
matibabu.
Mara
baada ya kuwasili katika Uwanja ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius
Nyerere wakiwa wameambatana na mama yao mzazi Grace Joel na Daktari
aliyekuwa akiwaangalia nchini India ambaye pia alikuwa masomoni akisomea
magonjwa ya Moyo kwa watoto Dkt. Glory Joseph wamepokewa na Mkuu wa
Kitengo cha Magonjwa ya Nje wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii Dkt.
Edward Sawe na baadhi ya wauguzi kutoka Taasisi ya Mifupa (MOI) .
Mapacha
hao wa kiume wakiwa wenye furaha na afya njema walichukuliwa katika
gari maalum na kupelekwa katika Taasisi ya Mifupa (MOI) ambako watakaa
kwa muda mfupi na kisha kuruhusiwa kuelekea wilayani Kyela jijini Mbeya
ambako ndiko walikozaliwa.
Kwa
upande wake mama mzazi wa watoto hao akizungumza kwa furaha mara baada
ya watoto wake kupatiwa matibabu ya kuwatenganisha kwa mafanikio makubwa
amesema kuwa sasa maisha yake yamebadilika na ataishi kwa furaha na
watoto wake.
“Najisikia
furaha sana kwa hatua niliyofikia mpaka hapa watoto wangu Eliudi na
Elikana sasa ni wazima naishukuru sana Serikali kupitia Wizara ya Afya
kwa msaada ilionipatia” amesema.
Kwa
uipande wake Daktari aliyekuwa akiwaangalia nchini India ambaye pia
alikuwa masomoni akisomea magonjwa ya Moyo kwa watoto Dkt. Glory Joseph
akizungumzia matibabu ya watoto hao nchini India amesema kuwa hatua ya
kuwatenganisha imekamilika na mwezi wa 8 mwaka huu watarudi tena nchini
India kwa ajili ya uchunguzi na matibabu zaidi ya afya zao.
“Ni
kwamba watoto hao wametenganishwa, kwa wakati huu wanaelekea MOI ambako
watakaa kwa muda na baadaye wataruhusiwa kwenda kwao Mbeya kujumuika na
jamaa zao” amesema.
Kwa
upande wake msemaji wa wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii Bw. Nsachris
Mwamwaja amesema kuwa watoto hao waliwasili jana jioni na ndege ya
shirika la ndege la Oman baada ya kumaliza matibabu ya awamu ya kwanza.
Amesema
upasuaji huo mkubwa wa kuwatenganisha watoto hao ulichukua saa 18 na
kufafanua kuwa kati ya hizo saa 13 zilitumika kutenganisha viungo
vilivyoungana sehemu ya chini ya uti wa mgongo,sehemu ya utumbo
mpana,njia ya mkojo,kibofu cha mkojo na sehemu za uume huku saa 5
zikitumika kuunganisha sehemu zilizotenganishwa.
“Kumbukumbu
zinaonyesha kuwa mpaka sasa duniani upasuaji wa aina hii umefanikiwa
mara tano kutenganisha mapacha watoto wa kiume walioungana”
amesisitiza.
Ameongeza
kuwa matibabu hayo ni juhudi za serikali katika kuhakikisha kuwa huduma
za afya zinatolewa kwa kila mwananchi kila inapowezekana na kutoa wito
kwa jamii kujenga utaratibu wa kuwafikisha mapema kwenye vituo vya afya
wale wote wenye matatizo ya kiafya badala ya kuwafikisha pindi hali zao
zinapokuwa mbaya.
0 Comments