REDD'S MISS TANZANIA 2012 , BRIGITTE ALFRED AWASHUKURU WATANZANIA

 

REDD’S Miss Tanzania 2012 -2013, Brigitte Alfred  akifafanua jambo kulia kwake ni Mkurugeni wa Kampuni ya Lino International Agency , ambao pia wanaratibu shindano hilo kwa mwaka wa 20 sasa , Hashim Lundenga, na kushoto ni Mkuu wa Itifaki Albert Makoye.
 
REDDS Miss Tanzania 2013 ambaye pia amefanikia  kushika nafasi ya tatu katika shindano la Mrembo na Malengo (Beauty With a Purpose) wakati wa kuwania taji la dunia (Miss World) mwaka huu shindano lililofanyika nchini Malaysia.

Brigitte alisema  hayo leo asubuhi katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika jijini Dar es Salaam mkwamba aliweza kushinda nafasi hiyo kupitia kazi zake za kijamii ambazo alifanya kwa kipindi cha mwaka mmoja ambapo aliweza kufanya mambo mbalimbali kwa watoto wenye ulemavu wa ngozi (Albino). 

"Video yangu ya kazi mbalimbali za kujitolea kwa kipindi cha mwaka mmoja ndizo zilizonifikisha katika nafasi hii kuku nafasi ya kwanza ikinyakuliwa na mrembo wa Nepal nay a pili kwenda kwa Miss Australia" alisema.

Kwa ushindi huo mrembo huyo amewashukuru Watanzania kwa kumuunga mkono kwa kipindi chote alichokuwa akishikilia taji hilo. 

Brigitte alifanikiwa kushika nafasi hiyo katika shindano hilo, ambalo lilishirikisha warembo zaidi ya 190 kutoka nchi mbalimbali duniani, ambalo lilikuwa mahususi kwa warembo kuonyesha kazi walizofanya kwa jamii katika nchi wanayotoka. 

Mrembo huyo alionyesha jinsi alivyosaidia kwa kiasi kikubwa kutoa msaada kwa watu wenye mahitaji maalumu hasa wale wenye ulemavu wa ngozi. 

Akizungumzia kuhusu shindano la  dunia alisema, lilikuwa na changamoto nyingi na anaamini ni lazima Watanzania wajivunie mafanikio ambayo yamefikiwa mpaka sasa katika mashindano hayo ya dunia. 

Mafanikio makubwa zaidi ambayo Tanzania iliwahi kuyapata ni kwa aliyekuwa Miss Tanzania 2005 Nancy Sumari alipofanikiwa kutwaa taji la Miss World Africa na kuwemo katika tano bora za warembo wa shindano hilo. 

 “Napenda kutoa shukrani zangu  za  dhati kwa Kamati ya Redd’s Miss Tanzania, wazazi wangu, vyombo vya habari, Serikali na Watanzania kwa ujumla kwa kuniunga mkono kwa kipindi chote hicho. 

“Kusema kweli sina cha kuwalipa na naahidi nitaendelea kushirikiana na kamati hii katika kuhakikisha Tanzania inafanya vyema zaidi katika mashindano ya dunia siku za baadaye,” alisema.

Wakati huohuo Mkurugenzi wa Kampuni ya Lino International, Hashim Lundenga ambao ndio waandaaji wa Redd’s Miss Tanzania alisema, wanajivunia kwa kiasi kikubwa mafanikio yaliyofikiwa na Brigitte katika mashindano hayo. 

“Kwetu tunachukua fursa hii kuyaomba makampuni au taasisi mbalimbali kujitokeza kudhamini mashindano haya kwani ni muhimu zaidi kwa ustawi wa Taifa,” alisema. 

Taji la Redd’s Miss Tanzania kwa sasa linashikiliwa na Happiness Watimanywa ambaye alifanikiwa kulitwaa hivi karibuni. 

Shindano la Redd’s Miss Tanzania linadhaminiwa na kinywaji cha Redd’s Original kinachozalishwa na kusambazwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL).

Post a Comment

0 Comments