STEVE NYERERE pichani naye kaachia ngoma japo anasema kwamba yeye anaimba kwa hobbie na siyo kusaka mahela.
Huenda, kutokana na mafanikio ya
aliyekuwa msanii wa filamu, Zuwena Mohammed ‘Shilole’, labda ndiko kumewapa
mshawasha wengine kujaribu kuimba kwa lengo la kupata mafanikio.
.............
WASANII
wengi hapa nchini, hususan wale wa filamu ‘Bongo Movie’ wengi wao wameibuka na
kutangaza kuacha kucheza filamu na kugeukia muziki wa Bongo Fleva.
Hii ni sawa,
lakini je ni kweli wana vipaji vya kuimba ama ni kutaka kuuza sura tu?
Ni jambo la
kawaida na zuri, kwa kila binadamu kuamua kuiga mambo mbalimbali yaliyo mazuri,
ikiwa ni njia moja katika kusaka maendeleo binafsi.
Lakini
katika hili, wasanii wa bongo movie, wengi wenu kugeukia muziki hiyo si sawa,
kwani inaonesha dhahiri kwamba, wengi wao wanafuata mkumbo.
Kwa kufuata
mkumbo huku, sina shaka kwamba, hata nyimbo watakazoziachia hazitakuwa na
mashiko kama jinsi ilivyo kwa wasanii ambao tangu awali waliamua kujikita
katika muziki.
Ushauri wa
safu hii ni kuwaomba wajidhatiti katika kuandaa filamu zao, ambazo kwa ukweli
usiopingika, nyingi zimekuwa zina upungufu mwingi ambao unahitaji marekebisho.
Lakini,
badala ya kufanya masahihisho katika filamu zao na kuondoa makandokando
yaliyomo, sasa wanageuza mwelekeo na
kukimbilia muziki, ambako nako sitarajii kama watatenda miujiza.
Nadhani,
laiti kama wakiamua kujikita ipasavyo katika filamu na kutuliza vichwa vyao,
sambamba na kupata mafunzo mbalimbali yanayohusu fani hiyo, huenda wangefika
mbali zaidi ya hapa walipo kwa sasa.
Inasikitisha
kuona kwamba, msanii ambaye alikuwa anafanya vema katika filamu, kisha
akageukia bongo fleva lakini anashindwa kufanya vizuri katika kuimba, hii
itaweza kumshusha hata katika mauzo ya filamu zake bila ya yeye kujua.
Usanii ni
pamoja na kukopi, lakini kwa kukopi kipaji cha mtu hii si sawa, kwani kila mtu
amezaliwa na kipaji na uwezo wake, hivyo kwa kulazimisha kipaji ambacho siyo
cha kwako, sidhani kama yupo ambaye atafanikiwa.
Huenda,
kutokana na mafanikio ya aliyekuwa msanii wa filamu, Zuwena Mohammed ‘Shilole’,
labda ndiko kumewapa mshawasha wengine kujaribu kuimba kwa lengo la kupata
mafanikio.
Kwa upande
wa Shilole, Mungu alimuumba na kumpa vipaji, kwani yeye alipotangaza kuwa muimbaji
wa Bongo Fleva, alitoka na Aboubakar Katwila ‘Q- Chillah’ na wimbo wa ‘Sitaki
Lawama’ akaonekana kama kabebwa, lakini
kwa kuwa ule ulikuwa ndiyo mwanzo, wengi wakasema acha tumpe nafasi.
Akaja
akaachia ngoma nyingine ‘Paka wa Baa’, hapo kila mtu akamkubali na sasa
anatamba na kibao cha ‘Nakomaa na Jiji’.
Hivi sasa,
Shilole ameweza kupata mialiko mingi na kufanya maonesho kwenye matamasha
mbalimbali ndani na nje ya nchi.
Jina la
Shilole, limekuwa kubwa na kazi yake inatambulika hata kama wapo ambao watasema
amebebwa, lakini ukweli ni kwamba, uwezo wake unaonekana dhahiri.
Cha
kushangaza kwa sasa ni hawa wasanii wengine wa filamu, kupanga mstari na
kutangaza nia ya kuingia katika bongo fleva.
Sawa,
tangazeni nia siyo vibaya, ila je mtaweza kumudu au mnadhani kuna mteremko
huko?
Muziki siyo
lele mama, lazima uwe na uhalisia na siyo mchezo wa maigizo kama jinsi
mlivyozoea huku wakati mwingine ‘mkikopi’ kazi za watu na kuziweka sokoni.
Safu ya
Busati, inawatahadharisha bila kificho, ingieni katika muziki lakini mje mkiwa
kamili.
Baadhi ya
wasanii ambao wametangaza kuimba ni pamoja na Wema Sepetu, Jokate Mwegelo, Aunt
Ezekiel, Rashida Wanjara, Mzee Magari, Rose Ndauka na wengineo wengi, lakini
hadi sasa hakuna kipaji chochote kimeonekana na kufanya vizuri.
0 Comments