Mjumbe wa
Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Riadhaa Tanzania (RT), Tullo Chambo
akimkabidhi cheti mmoja wa washiriki wa kozi ya ukocha ngazi ya kwanza, Mary
Christopher, kozi hiyo imeandaliwa na Chama cha riadha Mkoa wa Dar es Salaam
(DAAA), kwa ushirikiano na shirikisho hilo, iliyomalizika jijini Dar es Salaam. (Picha na Habari Mseto Blog)
Washiriki wa
kozi ya ukocha wa riadha ngazi ya kwanza wakiwa katika picha ya pamoja na
wakufunzi wao baada ya kukabidhiwa vyeti vyao na mgeni rasmi, Mjumbe wa Kamati
ya Utendaji ya Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), Tullo Chambo (wa tano kutoka
kushoto mstari wa nyuma), aliyemwakilisha Rais wa Shirikisho hilo, Anthony
Mtaka.
Na Elizabeth John
MAKOCHA wa riadha waliohitimu Kozi ya Ukocha
Ngazi ya Kwanza (Level One Coaches
Course), jijini Dar es Salaam, wametakiwa kwenda kufanyia kazi kivitendo
mafunzo waliyopata huku wakitanguliza kujitolea zaidi badala ya fedha.
Wito huo, ulitolewa lei wakati wa kufunga kozi hiyo
kwenye Shule ya Msingi Kibasila jijini Dar es Salaam na Mjumbe wa Kamati ya
Utendaji ya Chama cha Riadha Tanzania (RT), Tullo Chambo, aliyemwakilisha Rais
wa Shirikisho hilo, Anthony Mtaka.
Chambo, aliwataka walimu hao kuhakikisha uelewa
na utaalamu waliyoupata, unakuza mchezo huo na hasa shuleni ambako ndiko vipaji
viliko ili riadha iweze kupiga hatua zaidi ya sasa.
“Kama mnavyojua hakuna mchezo wowote ambao
hauanzii chini na kama tunahitaji kuwapata wanariadha bora, tunatakiwa kuanzia
chini viliko vipaji, hasa kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari,”
alisema Chambo huku akiwataka kuendelea kujitolea zaidi, badala ya kutanguliza
fedha zaidi katika kutoa ujuzi wao, jambo ambalo limekuwa likiwafanya baadhi ya
wadau kuwakimbia na kuwachukua watu wasio na ujuzi katika matukio mbalimbali ya
riadha ili kuepuka gharama.
Akijibu ombi la wakufunzi hao kutumika katika
mashindano mbalimbali yakiwamo ya Taifa, Chambo alisema, RT inawaenzi wataalamu
wake na itaendelea kuwatumia katika matukio mbalimbali ingawaje si wote kwa
pamoja.
Kwa upande wa mkufunzi, Samwel Tupa, ambaye
anatambulika na Shirikisho la Riadha la Kimataifa (IAAF), alisema mbali ya
mafunzo ya nadharia na vitendo ambayo walimu hao walifundishwa juu ya mchezo wa
riadha, pia wamejifunza falsafa ya michezo.
"Tumewafunza kuwajenga nguvu wanariadha,
makuzi na mabadiliko sambamba na utaratibu wa mazoezi," alisema Tupa na
kuwataka kwenda kuyafanyia kazi yale yote waliyofundishwa ili kuendeleza mchezo
huo hapa nchini, badala ya kwenda kujikweza kwa kupata vyeti hivyo, kitendo
alichofananisha sawa na kuweka chemli chini ya uvungu chumbani.
Kozi hiyo ilishirikisha waalimu 23 wa shule za Msingi
na Sekondari kutoka mikoa mitatu, Dar es Salaam, Lindi na Shinyanga, ambako
mbali na Tupa, wakufunzi wengine walikuwa ni Kapteni mstaafu, Lucas Nkungu na
Idd Mhunzi kutoka Chama cha Riadha Mkoa wa Dar es Salaam (DAAA).
0 Comments