AMIGOLAS AKIRI KUTIMKA TWANGA,ASHA BARAKA AMPA 5

Amigolas katikati akiimba Enzi zake akiwa  na bendi yake ya zamani Twanga Pepeta wakwanza kulia ni Kiongozi wa bendi hiyo Luiza Mbutu na kushoto ni Greyson Semsekwa wakiwa katika moja ya onesho.
BAADA ya kudumu katika bendi ya The African Stars ‘Twanga Pepeta’ Hamis Kayumbu ‘Amigolas’ ambaye pia ni kati ya wasanii waasisi wa bendi hiyo sasa amevunja ukimya na kukiri kuwa ameamua kugeukia muziki wa Hotelini ambao anaona utamlipa kwa sasa.
Amigolas mwenyewe amethibitisha hilo kwa kuzungumza na mwandishi wa habari hii kwamba ni kweli ameamua kuipa kisogo bendi yake ya zamani ‘Twanga Pepeta’ na kwamba hivi sasa yeye na bendi yake hajaitaja jina kuwa wanajipanga kuanza mazoezi na baadaye watazungumza na vyombo mbalimbali vya habari katika mkutano maalumu.
“Nikweli nimeanzisha bendi ambayo itakuwa ikipiga muziki katika hoteli mbalimbali pia tutakuwa tunaporomosha muziki kwenye kumbi mbalimbali ,lakini kwa sasa ni mapema sana kusema hilo hivyo tunajipanga kwani tunatarajia pia kwenda nje ya nchi kupiga muziki” alisema Amigolas.Aidha aliongeza kwa kusema kuwa  hadi leo, jana alikuwa bado hajawaaga viongozi wa ASET  lakinianaweka mambo yake sawa na atapanga kwenda kuaga rasmi.
Wakati akitimka kimyakimya itakumbukwa , Mwaka 2008 Amigolas alipanga kung’atuka katika bendi hiyo lakini akabaki , kadhalika mwaka jana alitangazwa na vyombo vya habari kuhama bendi hiyo huku uthibitisho wa kutosha kutoka kwake ukikosekana tofauti na mwaka huu ammbapo amekiri.
Mbali ya Amigo wasanii wengine  wanaounda bendi hiyo ni pamoja na Mpapasa Kinanda mahiri  Victor Mkambi na Rapa machachari Diouf.
Akizungumzia hilo  Mkurugeni wa Kampuni ya ASET , Asha Baraka alisema kwamba wanaahidi kumpa sapoti kubwa Amigolas, “Tutampa sapoti ya kutosha Amigo na tunamtakia kila la kheri aendako kwani muziki wa sasa ni mchakamchaka nay eye kutokana na umri pamoja na afya yake kwa sasa hawezi mbiombio zilizopo kama jinsi alivyokuwa zamani”.
Anaongeza kwa kusema kuwa zamani Amigo aliweza kufanya shoo kuanzia Jumatano, Alhamisi, Ijumaa, Jumamosi, Jumapili lakini kwa muda wa miaka miwili sasa hata katika bendi amekuwa akifanya shoo moja tu hivyo hadi hapo utaona kwamba alishabadilika na kwa staili aliyoichagua ya kuhamia katika muziki wa hotelini ataweza kwani ule hauna makeke sana” alisema Asha.

Post a Comment

0 Comments