MWANAMUZIKI msomi pichani kulia , anayetajwa kuwa mwanamuziki wenye tungo
zinazozusha misemo mingi mitaani, Hamis Mwinjuma, au Mwana FA ametaja sababu ya
kuliita onesho lake Litakalofanyika a Ijumaa hii kuwa maridhawa (The Finest)
kwani ni maadhimisho ya miaka 18 ya muziki wake ambao iwapo ungekuwa ni uhai wa
binadamu, basi angekuwa ameingia katika hatua ya utu uzima.
MwanaFA aliyasema hayo wakati alipoongea na baadhi ya
waandishi wa habari za burudani kuhusiana na tamasha lake hilo ambalo mwenyewe
analichukulia kama mahafali ya muziki wake kwani amepitia mambo mengi sana
mpaka kufikia hatua ya kuitwa MwanaFA.
"Nitaeleza kila kitu katika tamasha hili na hata
kuhusiana na tamasha langu la kwanza kupanda jukwaani huko Tanga, na nakumbuka
mpaka nguo nilizovaa siku hiyo, na mambo mengi watu watayapata kwa ufasaha
kuhusiana na mimi, hata hizi tetesi tetesi miongoni mwa mashabiki
ntazijibu", alisema MwanaFA.
Sababu nyingine aliyoitoa kuhusiana na ‘The Finest’ ni
kuhusiana na fursa kwa mashabiki wa muziki wa Hip Hop sasa kupata nafasi ya
kuhudhuria maonesho ya muziki huo yenye mtazamo wa kistaarabu, tofauti na
ilivyozoeleka.
Amesema kwa kipindi kirefu sasa imekuwa ikiaminika kwamba
Hip Hop ni muziki wa kihuni na wanaohudhuria muziki wa aina hiyo wanaitwa
masela na hata mavazi yao huwa ni filana na masuruali makubwa, na viatu vikubwa
jambo ambalo sasa linatakiwa kuondoka katika nafsi za watu kwani muziki
umeshakuwa biashara.
Ameieleza imani yake ya kwamba anaamini kuna watu na heshima
zao wanaupenda muziki huu lakini kutokana na mazingira wamekuwa wakikosa fursa
ya kuushuhudia jukwaani na hii ndio nafasi yake pekee.
MwanaFA anaamini kwamba Hip Hop ni muziki wa kimataifa
unaopatikana katika kila taifa tofauti na aina nyingine za muziki, ukiachilia
mbali reggae.
Akatoa mfano wa kundi la Wu Tang Clan ambalo hufanya ziara
zake mpaka China na kujaza mashabiki kiasi cha kuhatarisha usalama.
0 Comments