AIPS KUSAIDIA MAFUNZO YA WAANDISHI WA HABARI ZA MICHEZO TANZANIA



1
JUMA PINTO-MWENYEKITI TASWA

CHAMA cha Kimataifa cha Waandishi wa Habari za Michezo (AIPS),kimeahidi kusaidia masuala mbalimbali yahusiyo mafunzo kwa waandishi wa habari za michezo wa Tanzania.

Rais wa AIPS,Gianni Merlo raia wa Italia aliwapa fursa viongozi wa vyama vya waandishi wa habari za michezo wa Afrika kuwasilisha changamoto mbalimbali zinazovikabili vyama vyao, lakini kati ya hizo changamoto waitaje moja ambayo wanataka AIPS isaidie kuwapa msaada.
Tunashukuru Merlo kwanza alivutiwa sana na namna Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA) kinavyofanya kazi zake na ushiriki wake wa mikutano ya Dunia mara kwa mara, hali ambayo aliahidi yeye binafsi kusaidia chama chetu kuboresha masuala ya kimsingi.

Kubwa ambalo AIPS baada ya kuelezwa imesema italipangia utaratibu ni suala la mafunzo kwa waandishi wa habari chipukizi na wanawake kwani hayo ni baadhi ya mambo ambayo wenyewe wanayatilia mkazo na hasa baada ya kujulishwa kuwa kuna wanahabari zaidi ya 50 wanawake hapa nchini wanaofanya kazi kwenye masuala ya michezo.

Hata hivyo ingawa TASWA iliomba isaidiwe mafunzo kwa wanachama wake wote kwa kupatiwa wataalamu hasa wakati huu ambao kuna changamoto kubwa ya teknolojia ya habari na mawasiliano, lakini AIPS imesema kwa mwaka huu uwezo wake ni kwa waandishi wa habari za michezo chipukizi kupitia programu inayoandaliwa na AIPS.

Lakini Rais wa AIPS aliutaka ujumbe wa Tanzania utakapokuwa umerudi nyumbani umuandalie mikakati hiyo kwa mafunzo ya wanawake ili ikiwekezekana yafanyike kwa awamu katika kipindi cha miezi 18 kutegemea na idadi ya wahusika na pia gharama zenyewe. Nchi wanachama 103 duniani zikiwemo nchi 24 za Afrika zilihudhuria mkutano huo uliomalizika juzi Sochi, Urusi, ambapo pia ulifanyika uchaguzi wa viongozi wa AIPS watakaokuwa madarakani kwa miaka minne ijayo, ambapo Merlo alipita bila kupingwa.

Mkutano Mkuu wa AIPS ambao ni wa 76 ulimalizika juzi, ambapo kulikuwa na kikao cha makatibu wakuu wa kila nchi kilichoendeshwa na Katibu Mkuu wa AIPS, Roslyn Morris ambapo Tanzania iliwakilishwa na Katibu Mkuu wa TASWA, Amir Mhando na huko pia suala la tuzo mbalimbali zinazotolewa na wanahabari zilizungumzwa kwa kina.

Pia kulifanyika kikao cha marais wa AIPS wa mabara na baadhi ya viongozi wa vyama vya wanahabari wa michezo wa Afrika kilichokuwa chini ya Merlo, ambapo nilidhuria na ajenda kubwa ilikuwa suala la rushwa kwenye michezo na mambo ya upangaji wa matokeo wa mechi mbalimbali. Baada ya mkutano huo, wakati ujumbe wa Tanzania ukiwa njiani kurejea nyumbani ulipitia jijini Moscow, Urusi na kuzungumza masuala mbalimbali na Balozi wa Tanzania nchini Urusi, Jaka Mwambi.

Kwa ujumla mkutano ulikuwa na manufaa makubwa kwa Tanzania na Afrika kwa ujumla, ambapo masuala mengine mengi yaliyojitokeza kwenye mkutano huo ikiwemo namna ya mafunzo hayo yatakavyofanyika tutayazungumza Jumatano ijayo kwenye mkutano na wanahabari utakaofanyika ukumbi wa City Sports Lounge, Dar es Salaam saa tano asubuhi.

TASWA ni mwanachama hai wa AIPS yenye makao yake makuu Lausanne, Uswisi, ndiyo sababu kila mwaka tumekuwa tukishiriki mikutano hiyo tangu tulipoingia madarakani mwaka 2010.Mwaka 2011 tulishiriki Mkutano Mkuu wa AIPS uliofanyika Seoul Korea, Korea Kusini na tuliwakilishwa na Makamu Mwenyekiti, Maulid Kitenge na Katibu Msaidizi, George John
Pia tulishiriki Mkutano Mkuu wa AIPS uliofanyika Innsbruck, Austria Januari mwaka jana, ambapo Katibu Mkuu, Amir Mhando alihudhuria.

Post a Comment

0 Comments