LINDI, Tanzania
“Uteuzi wake umeanza rasmi Desemba 1 na tunaamini wadau wa LSA
watatoa ushirikiano kwake kama Msemaji katika kuhakikisha anatekeleza
majukumu yake ipasavyo, kwa ustawi wa kituo chetu”
UONGOZI wa Kituo cha Kuibua na Kuendeleza Vipaji vya Soka
Manispaa ya Lindi (Lindi Soccer Academy – LSA), kimemtangaza mwandishi wa
habari wa Kampuni ya Free Media Ltd inayochapisha magazeti ya Tanzania Daima na
Sayari, Salum Mkandemba (pichani kulia) kuwa Ofisa Habari wa kituo hicho.
Akizungumza na gazeti hili jana, Mkurugenzi wa LSA, Hafidh
Karongo alisema kuwa, uongozi, wazazi na wachezaji wamekubaliana kwa kauli
mmoja kumteua Mkandemba kuwa Msemaji wao, ili kuhakikisha anachangia katika
kukiletea maendeleo kituo hicho maarufu Kanda ya Kusini.
Aliongeza kuwa, wao kama LSA wanathamini mchango mkubwa wa
mwandishi huyo katika kukitangaza kitu nje ya mipaka ya mkoa na nchi, hali
iliyowafanya waamue kurejesha fadhila zao kwa kumpa nafasi hiyo, uteuzi
ulioanza rasmi Desemba 1.
“Uteuzi wake umeanza rasmi Desemba 1 na tunaamini wadau wa
LSA watatoa ushirikiano kwake kama Msemaji katika kuhakikisha anatekeleza
majukumu yake ipasavyo,” alisema Mkurugenzi huyo wa kituo hicho maarufu Kanda
ya Kusini inayojumuisha mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma.
Akizungumzia uteuzi huo, Mkandemba alisema kuwa,
anawashukuru LSA kwa kutambua mchango wake kiasi cha kuamua kumpa nafasi ya
kuwa sehemu ya kituo hicho, huku akiahidi kuhakikisha anatumia nafasi hiyo
kukiletea kituo maendeleo ngazi ya mchezaji mmoja mmoja na mkoa kwa ujumla.
Aidha, lile pambano lililokuwa lipigwe katika kilele cha
Siku ya Ukimwi Duniani, Desemba 1 kati ya LSA dhidi ya FC Toto ya Mtwara na
kusogezwa mbele kupisha hotuba ya Rais Jakaya Kikwetealiyekuwa mgeni rasmi wa
sherehe hizo kitaifa, lilipigwa jana kwenye Uwanja wa Ilulu.
Katika mechi hiyo uliyovuta hisia za wengi, LSA ilikubali
kichapo cha mabao 3-2. Wafungaji wa FC Toto katika mechi hiyo walikuwa ni
Faraji Namadila, Henry Galus na Ginoa Crispin, huku yale ya LSA yakiwekwa
nyavuni na Fabian Said na Abdul Shein.
0 Comments