MAREHEMU WILLY EDWARD KUZIKWANYUMBANI KWAO MUGUMU ,WILAYANI SERENGTETI LEO

Mwenyekiti wa Vyombo vya Habari Reginald Mengi akimzungumzia marehemu Willy siku alipoagwa 
Dar es Saam.
 Mhariri wa Gazeti la Uhuru Jane Mihanji
Mtoto wa marehemu  Tollman Willy Edward  akitoa heshima za mwisho kwa mwili wa baba yake.

PUMZIKA KWA AMANI  ‘NYOKA LONGO ’ WILLY EDWARD
Na Khadija Kalili
Makala hii imetoka katika gazeti la Tanzania aima la Juni 22,2012.
AHLAN WASAHLAN Mpenzi msomaji wa safu ya Busati. Karibu tena katika safu hii uipendayo yenye kukuburudisha mtima wako.
Mpenzi msomaji wangu kwa leo sitajadili mada ya burudani kama ilivyo kawaida ya safu hii, bali nitakushirikisha katika kumkumbuka mdau mkubwa wa tasnia ya michezo na burudani nchini, mwanahabari mwenzangu Willy Edward Ogunde aliyefariki ghafla Juni 16, mwaka huu, Mkoani Morogoro alikokokwenda kikazi.

Willy ambaye wakati akipatwa na mauti hayo alikuwa mhariri wa gazeti la Jambo Leo, binafsi nitamkosa siyo tu kwa sababu alikuwa mwandishi mwenzangu, bali  pia kwasababu alikuwa mshkaji wangu wa karibu ambaye tulikuwa tukisaidiana na kudadavua mambo mbalimbali yahusuyo maisha ya kila siku, kikazi, kifamilia, muziki na hata michezo.

Nitamkumbuka Willy ‘Fally Ipupa’, ‘Nyoka Longo'  ,‘Bawji Ogunde’ haya ndiyo  majina mengi ya utani niliyozoea kumwita hivyo ikiwa ni  kutokana na sifa moja kwangu ambayo wengi waliomfahamu watakubaliana nami kuwa alikuwa kijana mtanashati katika mavazi wakati wote.

Nakumbuka wapo marafiki zake ambao walikuwa wakimwita ‘Fally Ipupa’, lakini mimi nilikua nikimwita ‘Nyoka Longo’ na nilimbatiza jina hilo huku mwenyewe katika enzi za uhai wake akilifurahia na alikuwa akiitika pasina shaka.

Kwa muhtasari tu, wadau wangu ni hivi, wapo watakaoshtuka kwanini nilimfananisha na  Nyoka Longo, ni kwamba hilo ni jina la kiongozi wa bendi ya Zaiko Langa Langa, ya Kongo Kinshansa (DRC) hivyo nilimwita jina hilo kwa kwasababu tangu naaanza kumjua alikuwa na sifa za utanashati, alilipenda jina hilo na wakati wote nilipomuita jina hilo alitabasamu tu.
Nyoka Longo, pamoja na sifa ya uimbaji, pia alikuwa mtanashati kiasi kwamba alikuwa akinivutia kutokana na anavyokuwa anapiga ‘bling bling’ wakati wote, jinsi nilivyokuwa nikimwona katika Video zake zote.

Kama hiyo haitoshi, mimi na Willy tulifahamiana tangu mwaka 1998, ambapo nilikuwa mwandishi chipukizi, huku nikiwa besti mkubwa wa marafiki zake ambao ni Juma Pinto, Mobhare Matinyi  na Ben Kisaka.

Nitamkumbuka Willy kwa jinsi ambavyo tulikuwa tukifanya kazi kwa pamoja, licha ya kwamba hatukuwahi kuwa katika chumba kimoja cha habari, lakini aliweza kunisaidia kwa njia moja ama nyingine.

Nakumbuka  siku moja niliwahi kumwambia kuwa, nimeteuliwa kusimamia Makala za Burudani, lakini naona ni kama vile siwezi na muda wa kufanya hivyo kama bado kwangu.

Hiyo ilikuwa ni mwanzoni  mwa 2007, ambako Willy alikuwa ni kati ya watu  wangu wa karibu wachache walionipa moyo kuwa, hakuna kinachoshindikana chini ya jua , huku akinitakia mema na ufanisi katika kazi zangu na usimamizi wa dawati langu  la burudani ambalo nawajibika hadi sasa.

Hata pale nilipomweleza kuwa, kazi ya kupitia makala za burudani naifurahia kwakuwa , inanizalishia marafiki huku nikiichukia kwakuwa wakati huohuo inaniletea maadui pia, aliniambia hiyo ndiyo kazi na kuniasa kamwe nisirudi nyuma.

“Watakaokuchukia kwa sababu ya kazi waache tu, lakini iko siku watatambua umuhimu wako, wapotezee na wala wasikuumize kichwa,” alikuwa akiniambia.

Hakika ni marafiki wachache katika hii dunia wenye moyo kama Willy, wanaoweza kukuambia ukweli kwa utaratibu pale inapobidi, badala ya kukusema pembeni.

Sizungumzi haya eti kwa vile leo Willy amefumba macho, hasikii tena ‘ufagio’ huu, la, nimeamua kuanika kitu kilichokuwa kwa mpendwa huyo.

Alikuwa akinipa ujasiri wa kuwa na kifua cha kuvumilia maovu ninayotendewa kwa kunikataza kuchukua maamuzi ya hasira na ya jazba katika maisha.

Kwa sababu nilimchukulia kama kaka yangu, na mimi kwake nilikuwa ni dada rafiki, tuliweza kutembea katika  kumbi za burudani usiku  mara kadhaa na kuwa katika matamasha mbalimbali, huku kila mmoja akimlinda mwenzake hadi wakati wa kurudi nyumbani.

Kwakuwa alikuwa kijana baada ya kazi alipenda kujichanganya, nakumbuka aliipenda sana bendi ya Twanga Pepeta na hakukosa onesho  lolote la bendi hiyo katika  enzi za uhai wake , hivyo kila Jumatano alikuwa akipenda sana kutembelea Club Bilicanas tulikokuwa tukigongana mara kwa mara.

Nakumbuka wakati mwingine niliweza kumwambia aje na mkewe,  basi na mimi nikiwa na genge langu, tulijichanganya ipasavyo hadi muda ulipotaradadi.  

Kwa kweli, Nyoka Longo wangu, atabaki kuwa akilini, ambako nasema wazi upweke alioniachia, utaendelea kunitesa kila nukta ya saa itakayogonga.

Ni Willy ambaye alikuwa rafiki mpole, mwaminifu na ambaye nina hakika ametusitiri wengi  kwa mwengi , ulikuwa huwezi kuzungumza naye siri halafu akakusaliti kwa kuimwaga pembeni.

Lakini ndiyo hivyo tena, kazi ya Mola haina makosa, yeye ndiye alitoa na ndiye aliyetwaa, sisi wengine sote tuko nyuma yake.

Kumlilia  kwa machozi pekee  hakutoshi naamini hivyo kwakuwa kifo kimeumbwa kwa ajili ya kila kiumbe  kinachopumua chini ya mbingu hivyo namshukuru Mungu kwa yote na mapenzi yake. 

Bwana alitoa na Bwana ametwaa, jina la Bwana lihimidiwe, amwangazie mwanga wa milele, amina.

Post a Comment

0 Comments