KILIMANJARO PREMIUM LAGER NA BASATA WATANGAZA VIINGILIO TUZO ZA KILI VIP SH.75,000 &20,000


Meneja wa Bia ya Kilimanjaro, George Kavishe aikizungumza na waandishi wa habari, Dar es Salaam leo asubuhi  kuhusu Sherehe za Tuzo za Kilimanjaro Muziki 2012 zitakazofanyika katika Ukumbi wa Mlimani City, Aprili 14. 

VIINGILIO kwa ajili ya hafla ya utoaji wa Tuzo za Muziki Tanzania itakayofanyika kwenye ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam Aprili 14, mwaka huu vimetangazwa, ambapo cha juu ni sh 75,000 huku cha chini kikiwa ni sh 20,000.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Meneja wa Bia ya Kilimanjaro, ambao ndio wadhamini wa tuzo hizo, George Kavishe, alisema kiingilio cha sh 75,000 ni maalumu kwa siti maalumu, ambapo pia kutakuwa na chakula cha usiku, vinywaji bia na mvinyo, huku siti za kawaida ni sh 20,000 na bia ya Kilimanjaro.

Kavishe alisema usiku huo wa utoaji tuzo kwa wasanii, utasindikizwa na wasanii wa nyumbani, ambao ni Diamond, kundi la TMK Wanaume, Charles Baba, Khalid Chokoraa, Recho, Ommy Dimples na Hassan Bichuka.

Aidha, Kavishe alitoa shukrani kwa Watanzania, kujitokeza kwa wingi katika zoezi la kuwapigia kura wasanii wanaotaka washinde tuzo hizo.

“Tumevuka lengo la idadi ya kura kwa nyanja zote, ikiwa ni maana ya ujumbe mfupi, vipeperushi, barua pepe na mitandao, hii inamaanisha tuzo zimekubalika na zimepokewa vizuri,” alisema.
Pia Kavishe amelishukuru Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), kwa kuendelea kutoa ushirikiano kwa bia ya Kilimanjaro na kuipa tena kibali cha kudhamini na kuendesha shughuli za Tuzo za Muziki Tanzania.

Tiketi hizo zitauzwa kuanzia Jumatatu ijayo, Mlimani City, Baraka Garden Posta, Mtaa wa Azikiwe, Zizzou Fashion ya Victoria, Sinza na Tegeta, Born to Shine Mwenge, Robbie One Fashion Kinondoni na Engine Petrol Station Mbezi.

Post a Comment

0 Comments