WAWILI WAINGIA JOPO LA WAKUFUNZI CAF
Watanzania Leslie Liunda na Joan Minja wamechaguliwa kuwa wakufunzi wa waamuzi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) baada ya kufaulu katika kozi iliyofanyika Mei mwaka jana jijini Cairo , Misri.
Minja ambaye pia ni Katibu wa Kamati ya Waamuzi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na Liunda ni miongoni mwa zaidi ya waamuzi wa zamani 90 walioshiriki kozi hiyo ambapo jumla ya waliofaulu na kupata ukufunzi wa CAF ni 58 wakiwemo wanawake tisa.
Ukanda wa CECAFA (Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati) umetoa jumla ya wakufunzi tisa kutokana na kozi hiyo.
Wakufunzi hao kwa upande wa wanawake ni Minja (Tanzania ), Gladys Waweru (Kenya ) na Catherine Adipo (Uganda ). Kwa upande wa wanaume ni Liunda (Tanzania), Ali Waiswa (Uganda), Bernard Mfubusa (Burundi), Eshetu Sheferaw (Ethiopia), Jumaa Kaluwe (Kenya) na Salih Mohamed (Sudan).
Watanzania wengine ambao waliwahi kuwa wakufunzi wa waamuzi wa CAF ni Gratian Matovu, Joseph Mapunda na Alfred Lwiza.
MTANZANIA AOMBEWA ITC UINGEREZA
Chama cha Mpira wa Miguu Uingereza (FA) kimetuma maombi Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kumuombea Hati ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC) mchezaji Douglas Didas Masaburi ili ajiunge na klabu ya nchini humo.Masaburi mwenye umri wa miaka 21 anaombewa ITC ili ajiunge na klabu ya Coventry Spartans akiwa mchezaji wa ridhaa.
Coventry Spartans iko katika Ligi Daraja la Pili ya Midland . Mchezaji huyo anaombewa ITC kutoka katika klabu ya New Rule Power.
TFF inafanyia kazi maombi hayo na hati hiyo itatolewa mara baada ya taratibu husika kukamilika.
WAZAMBIA KUICHEZESHA TWIGA STARS UGENINI
Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limeteua waamuzi kutoka Zambia kuchezesha mechi ya kwanza ya mchujo ya Kombe la Afrika kwa Wanawake (AWC) kati ya Tanzania (Twiga Stars) na Namibia .
Mechi ya kwanza itachezwa jijini Windhoek , Namibia kati ya Januari 13, 14 na 15 mwakani. Mwamuzi ni Gladys Lengwe wakati waamuzi wasaidizi ni Patience Mumba na Mercy Zulu.
Mwamuzi wa akiba (mezani) atakuwa Bookanang Lekgowe kutoka Botswana wakati kamishna wa mechi hiyo kutoka Afrika Kusini atakuwa Smith Hilton Fran.
Mechi ya marudiano itachezwa Januari 29 mwakani Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam .
Twiga Stars inayofundishwa na kocha Charles Boniface Mkwasa akisaidiwa na Nasra Mohamed imeanza rasmi mazoezi jana (Desemba 19 mwaka huu) kwa ajili ya mechi hiyo.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
0 Comments