AFANDE TIBAIGANA AMUWEKA LOUIS SENDEU CHINI YA UANGALIZI NA KUMCHAPA FAINI YA SH 5000,000

Kamati ya Nidhamu na Usuluhishi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) inayoongozwa na Kamishna wa Polisi mstaafu Alfred Tibaigana imempiga faini ya sh. 500,000 na kuwekwa chini ya uangalizi kwa miezi sita Ofisa Habari wa Yanga, Louis Sendeu baada ya kumuona ana hatia kwa mashtaka yaliyowasilishwa dhidi yake na TFF.


Uamuzi wa kamati hiyo iliyokutana leo (Septemba 24 mwaka huu) umetokana na ushahidi uliowasilishwa na TFF, na pia Sendeu mwenyewe kukiri kuwa alifanya makosa.

Sekretarieti ya TFF ilimshtaki Sendeu kwenye kamati hiyo kutokana na matamshi yake dhidi ya mwamuzi Alex Mahagi mara baada ya mechi kati ya Yanga na Ruvu Shooting iliyochezwa Septemba 10 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kumalizika kwa sare ya bao 1-1.

Sendeu aliita mkutano na waandishi wa habari na kumshutumu Mahagi kuwa alisababisha timu yake ikose ushindi kwa kuwabeba wapinzani wao na kudai anamfahamu Mahagi kuwa ni mwanachama wa Simba, kadi nyekundu aliyompa kiungo wao Haruna Niyonzima si halali na alifanya hivyo kwa lengo la kuisadia Simba ili iendelee kukaa kileleni mwa ligi.

Kauli hiyo ililenga kumjengea chuki Mahagi mbele ya mashabiki wa Yanga kama ilivyo kwa viongozi na watendaji wa TFF wakati Sendeu akiwa ofisa wa Yanga alikuwa anajua taratibu za kufanya pale klabu yake isiporidhishwa na uamuzi wa mwamuzi au suala lingine lolote.

Kamati hiyo haikusikiliza mashtaka dhidi ya Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage kwa vile hakufika kwenye kikao kutokana na kuwa katika kampeni za uchaguzi za Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwania ubunge wa Jimbo la Igunga mkoani Tabora.

Pia kamati hiyo haikusikiliza mashtaka ya kwanza ya Sendeu kwa vile yanakwenda pamoja na yale ya Rage. Kamati itapanga tarehe nyingine kwa ajili ya kusikiliza mashtaka dhidi ya viongozi hao ambapo watapewa taarifa.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

Post a Comment

0 Comments