MABINGWA WATETEZI YANGA NA MAKAMU BINGWA KUKIPIGA USIKU WA AGOSTI 17

Mechi ya Ngao ya Jamii (Community Shield) kufungua msimu mpya wa Ligi Kuu ya Vodacom kati ya mabingwa watetezi Yanga na Makamu Bingwa Simba itachezwa usiku (Agosti 17 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Uamuzi wa mechi hiyo kuchezwa kuanzia saa 2.00 usiku umetokana na sababu kadhaa, kubwa zikiwa mbili; Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhan na pia Agosti 17 mwaka huu kuwa ni siku ya kazi.
Pambano hilo litatanguliwa na mechi ya vikosi vya pili (U20) vya timu hizo ambayo yenyewe itaanza saa 10.30 jioni. Mechi ya Ngao ya Jamii baada ya dakika 90 kama mshindi hatapatikana, zitaongezwa dakika 30. Katika muda huo nao kama mshindi atakuwa bado hajapatikana, itatumika mikwaju ya penalti.
Mechi hiyo imepata mwekezaji (Bigbon) na hivi sasa wadau wake wakuu- Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na klabu husika ziko katika mazungumzo ya mwisho mwekezaji huyo. Kwa redio ambazo zinataka kutangaza mechi hiyo moja kwa moja zinatakiwa kuwasiliana na Idara ya Habari na Mawasiliano ya TFF ili kupewa masharti ya kufanya hivyo.
Pia unafanyika utaratibu wa kuuzwa futari uwanjani mara baada ya mechi ya vikosi vya pili ili kuwawezesha washabiki waliofunga kutohangaika kutafuta sehemu ya kufuturu.
KAMATI TFF YAMREJESHA MCHAKI
Kamati ya Uchaguzi ya TFF ilikutana Agosti 10 na 11 mwaka huu kujadili rufani ya Frank Mchaki kupinga uamuzi wa Kamati ya Uchaguzi ya Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) kumuengua kugombea nafasi ya Katibu Mkuu katika uchaguzi wa Chama cha Mpira wa Miguu Wilaya ya Kinondoni (KIFA).
Chini ya Mwenyekiti wake Deogratias Lyatto, Kamati ya Uchaguzi ya TFF ilibaini kuwa pingamizi lililowekwa dhidi ya Mchaki na kujadiliwa na Kamati ya Uchaguzi ya DRFA, liliwasilishwa, kujadiliwa na kutolewa uamuzi kinyume na Kanuni za Uchaguzi za wanachama wa TFF Ibara ya 11(2) na (3) kwa kutotanguliwa na pingamizi mbele ya Kamati ya Uchaguzi ya KIFA, hivyo rufani hiyo haikuwa na sifa ya kusikilizwa na kutolewa uamuzi na Kamati ya Uchaguzi ya TFF. Hata hivyo baada ya kupitia kiini cha pingamizi, Kamati imefikia uamuzi kuwa tuhuma zilizotolewa dhidi ya mrufani zimekosa ithibati.
Kutokana na maelezo hayo, Kamati imekubaliana na rufani ya mrufani (Mchaki) dhidi ya uamuzi wa Kamati ya Uchaguzi ya DRFA, hivyo imemrejesha kugombea nafasi ya Katibu Mkuu wa KIFA.
Kwa kuzingatia Kanuni za Uchaguzi za wanachama wa TFF Ibara ya 8(3) Kamati ya Uchaguzi ya TFF inauahirisha uchaguzi wa KIFA uliokuwa ufanyike kesho (Agosti 13 mwaka huu) na sasa utafanyika Agosti 20 mwaka huu.
USAJILI LIGI DARAJA LA KWANZA
Usajili wa wachezaji wa klabu za Ligi Daraja la Kwanza kwa msimu huu utafanyika baada ya kumalizika Ligi ya Taifa hatua ya fainali inayoendelea hivi sasa kwenye Uwanja wa Mkwakwani, jijini Tanga.
Baada ya fainali hizo kumalizika Agosti 14 mwaka huu TFF itatoa mwelekeo wa usajili huo (roadmap) ikiwemo tarehe ya kuanza na kumalizika, pamoja na kipindi cha pingamizi. Timu tano kutoka kwenye fainali ya Ligi ya Taifa inayoshirikisha timu 12 zitapanda kuingia daraja la kwanza.
Ligi Daraja la Kwanza ambayo itaanza katika hatua ya makundi na baadaye kuchezwa kwa mtindo wa nyumbani na ugenini itashirikisha jumla ya timu 18, na inatarajia kuanza Septemba 3 mwaka huu.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

Post a Comment

0 Comments