FID Q AFIKISHA KILIO CHAKE KWA GHONJE MATEREGO

Msanii wa Hiphop nchini,Fareed Kubanda aka Fid Q akiwasilisha mada kuhusu Maudhui ya Hiphop na nafasi yake katika Jamii kwenye Jukwaa la Sanaa linalofanyika kila Jumatatu kwenye Ukumbi wa BASATA.Kulia kwake ni Msanii Zavala na Katibu Mtendaji wa BASATA,Ghonche Materego.
Katibu Mtendaji wa BASATA,Bw.Materego akisisitiza jambo wakati akihitimisha Jukwaa la Sanaa linalofanyika kwenye Ukumbi wa Baraza hilo kila wiki.Wengine kutoka kulia ni Msanii Fid Q na Zavala.

Msanii Zavala akijibu hoja mbalimbali kutoka kwa wadau wa Jukwaa la Sanaa juu ya Maudhui ya Muziki wa Hiphop na nafasi yake katika Jamii yetu.

Mdau akichangia mada kwenye mjadala huo.

FID Q ALIA NA TAFITI KWENYE MUZIKI WA KIZAZI KIPYA
Na Mwandishi Wetu
Msanii wa muziki wa kizazi kipya anayetamba katika miondoko ya Hiphop,Fareed Kubanda aka Fid Q ametoa wito kwa wadau wa sanaa hasa waandishi kujikita katika kuandaa machapisho na vitabu vinavyoelezea undani wa muziki huo.
Wito huo umekuja wakati ambao hakuna tafiti zinazofanywa katika muziki huo hapa nchini kiasi cha kutokuwepo kwa historia ya moja kwa moja inayoeleza asili ya muziki huo na nini hasa kilitokea hadi vijana wengi kujikita katika muziki huo ambao kwa sasa umepata umaarufu mkubwa.
Akizungumza kwenye Jukwaa la Sanaa wiki hii,Fid Q alisema kwamba,kumekuwa na ongezeko la watu kutoka nje wanaokuja kufanya utafiti kwenye muziki huu na kuondoka nao lakini waandishi na wadau wa sanaa wa ndani wamelala katika hilo na hawajaona fursa hiyo.
“Muziki huu una historia kubwa hapa nchini,watu wengi wanakuja kufanya utafiti,kuandika vitabu na kujizolea fedha.Hapa kwetu waandishi hawajaona haja ya kufanya hivyo.Wanaandika mambo madogo binafsi na kutojikita kwneye undani wa muziki huu”alilalamika Fid Q.
Aliongeza kwamba,kama juhudi za makusudi hazitaelekezwa katika kufanya tafiti na kutunza kumbukumbu za kutosha katika eneo hili,basi vizazi vitakosa kitu adhimu cha kukumbuka na kurithi.
“Tuna makundi mengi yalikuwepo kama Kwanza Unit na baadaye Hard Brastarz.Yalifanya kazi kubwa kusimamisha muziki huu hasa Hiphop nani anakumbuka? Tunahitaji kuweka mambo haya katika maandishi.Ni ajabu kukosa maandiko na tafiti katika mambo haya” alisisitiza
Kwa upande wake muasisi wa muziki huu na mwanzilishi wa moja ya makundi ya mwanzo katika muziki wa kizazi kipya la Kwanza Unit, Zavala alisema kwamba,wageni ndiyo wamekuwa wakihangaika na tafiti katika muziki huu lakini kwa waandishi wa nyumbani bado.
“Watu wanachota mamilioni katika kuandika miradi na tafiti kwenye muziki huu.Inashangaza hakuna waandishi waliokwisha kujitokeza kuandika vitabu na kufanya tafiti katika eneo hili linalovuta maelfu ya vijana” alilalamika Zavala.
Akihitimisha mjadala Katibu Mtendaji wa BASATA,Ghonche Materego alisema kwamba,ni vema waandishi na wasanii wakajikita katika eneo la muziki wa kizazi kipya kwani hakuna machapisho na vitabu vya kutosha.

Post a Comment

0 Comments